Pemba. Makamu Mwenyeti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Zainab Khamis Shomar amewataka wanafunzi walioathiriwa na janga la moto katika Shule ya Sekondari Fedel Castro kutokuvunjika moyo bali waongeze juhudi katika masomo yao sambamba na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuzima ndoto zao.
Shomar ametoa kauli hiyo leo Aprili 28, 2026 wakati akizungumza na wanafunzi wakati akiwafariji pamoja na kuwapatia msaada wa vitu mbali mbali na fedha taslimu Sh2 milioni, kufuatia janga la moto lililoteketeza bweni la wasichana Aprili 16, mwaka huu.
Amesema wanafunzi wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi katika mazingira yao na wapo wengi ambao hushindwa kufikia malengo yao kutokana na vishawishi mbalimbali.
Amesema sasa wanafunzi wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika masomo ili kuhakisha wanapata matokeo mazuri na wanatimiza malengo yao.
Amesema tukio hilo lisiwe kikwazo cha kuendeleza masomo yao bali juhudi zaidi zinahitajika kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Makamu Mwenyekiti (UWT) Taifa Zainab Shomar akiwafariji wasichan wa Skuli ya Fidel Casro baada ya kupoteza vitu vyao kwa kuunguliwa na moto kwenye bweni la kusomea.
“Niwaombe wanafunzi tukio hili lisiwakatishe tamaa mkajisikia wanyonge, bali mnapaswa kukaza kamba kuhakikisha mnafanya vizuri kwenye masomo yenu, sisi tumekuja kurejesha vitu vyenu vilivyoungua moto,” amesema.
“Tumekuja kuwafariji na kuwatia moyo msome na muepuke mambo ambayo yanaweza kuzima ndoto zenu,” amesema Shomar.
Aidha amewasisitiza walimu kuendelea kuwasimamia wanafunzi hao kuhakikisha wanafunzi wanaepukana na mambo yasiyokubalika katika masomo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Zukhra Mgeni Othman amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kuwafariji wanafunzi hao kufuatia mtihani walioupata hivi karibuni.
Amesema misaada hiyo waliyoitoa imerejesha imani na matumaini ya wanafunzi hao kuendeleza masomo katika hali ya utulivu wa nafsi.
“Serikali ya wilaya na mkoa inawashukuru wadau wote waliojitokeza kuwafariji wanafunzi waliofikwa na maafa hao,” amesema.
Awali Mratibu Idara ya Elimu Sekondari, Tareh Khamis Hamad amesema Wizara ya Eimu inafarajika na ushirikiano wa wadau, wamejitokeza kwa kuguswa na tukio hilo na kusaidia wanafunzi hao katika kipindi hiki kigumu.