Dar es Salaam. Wakati mabadiliko ya tabianchi yakiendelea kuvuruga maisha ya jamii mbalimbali, wanawake nchini Tanzania wameanza kujitokeza kwa nguvu mstari wa mbele, wakibuni na kutumia mbinu za ustahimilivu kukabiliana na athari zake katika maisha ya kila siku.

Kuanzia kukabiliana na ukame wa muda mrefu hadi athari za mafuriko, wanawake hasa katika jamii zinazotegemea kilimo na rasilimali za asili wamekuwa wakibuni njia mbadala za kuhakikisha familia zao zinaendelea kuishi licha ya hali ngumu na isiyotabirika ya mazingira.

Hata hivyo, pamoja na mchango huo mkubwa, sauti za wanawake zimekuwa hazisikiki vya kutosha, hali inayochochea juhudi mpya za kuanzisha majukwaa ya kuibua na kusambaza uzoefu wao pamoja na suluhisho wanazobuni wenyewe.

Katika kukabiliana na pengo hilo, Taasisi ya My Legacy imeanzisha mradi mpya unaotumia ubunifu na sanaa kuangazia uzoefu wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mradi huo unaojulikana kama Miale ya Kijani, unatarajiwa kuwashirikisha wanawake katika utengenezaji wa filamu fupi zinazosimulia hadithi zao halisi, zikionesha changamoto za kimazingira wanazokutana nazo katika jamii zao pamoja na mbinu wanazotumia kuzikabili.

Akizungumza leo Aprili 28,2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha wadau wa maendeleo, mazingira, sanaa, asasi zisizo za serikali (CSOs) pamoja na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa My Legacy, Fortunata Temu, amesisitiza umuhimu wa kuwapa wanawake nafasi ya kujieleza wenyewe.

“Wanawake wanakumbana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kiwango kikubwa, lakini pia wako mstari wa mbele katika kukabiliana nazo. Ni muhimu wakapewa nafasi ya kueleza uhalisia wao na suluhisho wanazobuni,” amesema.

Kwa upande wake, Magdalena George amesema wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na nafasi zao katika kaya na jamii.

Amesema licha ya changamoto hizo, wanawake wameendelea kuonesha ustahimilivu kwa kutumia mbinu bunifu, hasa katika sekta ya kilimo.

Akitolea mfano mkoa wa Dodoma, amesema baadhi ya wanawake wameanza kutumia mbinu za umwagiliaji wa matone, zinazowawezesha kutumia maji kidogo kwa ufanisi na kuendelea kuzalisha mazao hata wakati wa ukame.

“Hii inaonesha kuwa jamii zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho. Wanawake wanaongoza katika ubunifu huu na juhudi zao zinapaswa kutambuliwa na kuungwa mkono,” amesema.

Meneja wa Programu wa mradi wa Vijana at Work unaotekelezwa na CIDEA kwa kushirikiana na CT Institute na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), Mandolin Kahindi, ameeleza kuwa sanaa ina nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko ya kijamii.

Amesema kupitia majukwaa ya ubunifu kama filamu, maigizo na redio za jamii, vijana wanaweza kuongeza uelewa na kushirikisha jamii katika masuala mtambuka yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia na uhuru wa kujieleza.

“Tunaamini ushirikiano ni muhimu. Ndiyo maana tunahimiza ushirikiano kati ya vijana wenyewe na pia kati yao na mamlaka za serikali za mitaa ili kukabiliana na changamoto hizi na kuleta maendeleo,” amesema.

Juhudi kama mradi wa Miale ya kijani zinatarajiwa kuimarisha hatua hizi kwa kusaidia kuibua simulizi za wanawake, hatua itakayohamasisha jamii kujifunza, kubadilika na kuchukua hatua katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi badala ya kubaki katika hali ya kukata tamaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *