Njombe. Zaidi ya nusu ya waajiri nchini hawajajisajili katika Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), licha ya kuwepo kwa zaidi ya maeneo ya kazi 200,000.
Hayo yameelezwa leo, Jumanne Aprili 28, 2026, na Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mjimwema, mkoani Njombe.
Waziri Sangu amesema usajili wa maeneo ya kazi si suala la hiyari, bali ni takwa la kisheria, akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waajiri wanaoendelea kukiuka sheria hiyo.
“Watu wengi hawataki kujisajili licha ya kuwepo kwa zaidi ya maeneo ya kazi 200,000, lakini hata nusu yake haijafikiwa. Hili si suala la hiari bali ni la kisheria. Tutakuja na kampeni maalumu kuhakikisha usajili unafanyika,” amesema.
Ameongeza kuwa Desemba mwaka jana aliipa Osha siku 90 kuhakikisha waajiri ambao hawajajisajili wanafanya hivyo, lakini katika kipindi hicho walifanikiwa kusajili waajiri 4,000 pekee. Kutokana na hali hiyo, serikali imetoa tena siku 90 nyingine kwa waajiri hao kujisajili kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mbali na hilo, Waziri Sangu amesema baadhi ya waajiri katika sekta binafsi hawasajili wafanyakazi wao katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, akitoa pia siku 90 kwa utekelezaji wa hilo kabla ya hatua kali kuchukuliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba, akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo ya Osha yaliyofanyika mkoani Njombe.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuiwezesha Osha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikieleza kuwa tayari imetoa Sh7 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali, yakiwamo magari zaidi ya 40 ili kuongeza uwezo wa utendaji wa taasisi hiyo.
Akizungumzia maadhimisho hayo, Waziri Sangu amewashukuru wananchi wa Njombe kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuwakaribisha kushiriki pia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yatakayofanyika mkoani humo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda amesema maadhimisho ya usalama na afya mahali pa kazi hufanyika kila mwaka duniani kote, yakifikia kilele Aprili 28. Amesema chimbuko lake linahusishwa na mapinduzi ya viwanda, ambapo uzalishaji uliongezeka lakini usalama wa wafanyakazi ukapuuzwa.
Amesema mwaka 1996 kulifanyika maandamano makubwa jijini New York, Marekani ya kuwakumbuka wafanyakazi waliopata ajali, magonjwa na ulemavu kazini na mwaka 2001, dunia ilitambua rasmi umuhimu wa siku hiyo.
Kwa Tanzania, amesema maadhimisho hayo yalianza mwaka 2003 yakilenga kuhamasisha waajiri kulinda afya na usalama wa wafanyakazi. Katika maadhimisho ya mwaka huu, OSHA imewafikia wajasiriamali 6,101 na maofisa usafirishaji 300 kwa kuwapatia elimu na vifaa kinga, pamoja na kuendesha kliniki maalum za uchunguzi na matibabu.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya, amewahimiza wafanyakazi kutoa taarifa endapo hawataona uthibitisho wa usajili wa Osha katika maeneo yao ya kazi ili hatua zichukuliwe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba amesema uwekezaji katika usalama na afya mahali pa kazi si gharama bali ni msingi wa kuongeza tija, ufanisi na uendelevu wa biashara.
Akinukuu taarifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2026, Ndomba amesema hatari za kisaikolojia kazini, ikiwemo msongo wa mawazo husababisha upotevu wa takribani asilimia 1.37 ya pato la taifa duniani kila mwaka, hasara inayoweza kuepukika kwa kuwekeza katika mazingira salama ya kazi.