
Arusha. Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), umesema kuongezeka kwa shinikizo la kisheria na kiutendaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali, kunaendelea kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uwezo wa wanahabari kuripoti kwa uhuru masuala ya msingi ya kitaifa.
Kutokana na hali hiyo, umoja huo umeitaka serikali kuhakikisha inalinda usalama wa wanahabari, kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kuepuka matumizi ya sheria na kanuni kama nyenzo ya kuzuia haki ya msingi ya wananchi kupata taarifa.
Aidha, CoRI imevitaka vyombo vya dola kuacha vitendo vya vitisho na unyanyasaji dhidi ya wanahabari na badala yake, kusimamia sheria kwa usawa bila kudhoofisha uhuru wa kujieleza.
Akizungumza leo Jumanne Aprili 28, 2026, jijini Arusha kuelekea maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika Mei 3, 2026, Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura amesema bila vyombo vya habari vilivyo huru na salama, taifa linahatarisha kupoteza moja ya nguzo muhimu katika kulinda uwazi, haki na demokrasia.
Amesema shinikizo linaloongezeka limeanza kuathiri uwezo wa wanahabari kuripoti kwa uhuru, hata katika masuala nyeti ya kitaifa, jambo linalozua wasiwasi kuhusu mustakabali wa demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.
CoRI pia imelaani mwenendo huo unaohusishwa na baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na vyombo vya usalama.
Sungura amesema katika kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2026, matukio manane ya madhila dhidi ya wanahabari yameripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya na Mwanza.
Amefafanua kuwa matukio hayo yanajumuisha kukamatwa kwa wanahabari wanane na Jeshi la Polisi, kushikiliwa vituoni, kunyang’anywa vifaa vya kazi na mmoja kupewa saa 24 kujieleza kuhusu kauli alizotoa katika mahojiano ya chombo cha habari.
Pia, chombo kimoja cha habari kinaendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa kwa siku 90.
Kwa mujibu wa Sungura, hali hiyo inachochea hofu katika vyumba vya habari na kuibua tabia ya wanahabari kujidhibiti, jambo linalodhoofisha zaidi uwezo wa vyombo vya habari kuripoti kwa kina masuala yanayohusu uwajibikaji, utawala bora na maendeleo ya jamii.
Takwimu za CoRI zinaonyesha katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, jumla ya matukio 55 ya madhila dhidi ya wanahabari, vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa yameripotiwa, hali inayoashiria kuwa changamoto hiyo bado inaendelea licha ya maboresho ya sera na sheria.
Sungura ameonya kuwa shinikizo dhidi ya sekta ya habari lina athari kubwa kwa ujenzi wa demokrasia, kwa sababu hupunguza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati, kudhoofisha uwajibikaji wa viongozi na kuathiri ushiriki wa wananchi katika michakato ya maendeleo na maamuzi ya kitaifa.
Aidha, amesema hali hiyo inaweza kuathiri taswira ya nchi na juhudi za kukuza uhuru wa kujieleza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa), Edwin Soko amesisitiza umuhimu wa vyombo vya usimamizi kutekeleza sheria na kanuni kwa haki bila kuathiri uhuru wa kujieleza.
Pia, amewataka wadau wa sekta ya habari na wananchi kwa ujumla kuendelea kutetea haki ya kupata taarifa kama msingi muhimu wa demokrasia.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu amesema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yataanza rasmi Aprili 29, 2026, jijini Arusha, yakitarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Amesema mada mbalimbali zitawasilishwa wakati wa maadhimisho hayo, zikilenga kujadili uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari na mustakabali wa tasnia ya habari nchini.