
Dar es Salaam. Gharama za huduma za afya kwa wajawazito zinaendelea kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri upatikanaji na matumizi ya huduma muhimu za afya kwa mama na mtoto, hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Tafiti za afya ya umma zinaonyesha kuwa tozo za ada katika huduma za uzazi huchangia kwa kiwango kikubwa ucheleweshaji au hata kutokuwepo kabisa kwa matumizi ya huduma za msingi, ikiwamo uchunguzi wa awali wa ujauzito, kujifungua salama pamoja na huduma baada ya kujifungua.
Kihistoria, ada za huduma za afya ziliwahi kuhalalishwa kama mkakati wa kuchangia uendelevu wa mifumo ya afya na kuboresha ubora wa huduma, hasa katika mazingira yenye uhaba wa rasilimali za kifedha.
Hata hivyo, ushahidi wa kisayansi na uzoefu wa kimataifa vimebaini faida zinazotarajiwa za mfumo huu hazizidi madhara yanayotokana na kuweka mzigo wa kifedha kwa wajawazito, kundi ambalo tayari liko katika hatari kubwa ya kiafya na kijamii.
Kwa sasa, kuna mwafaka mpana miongoni mwa wadau wa afya, likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wa maendeleo, kwamba huduma muhimu za afya kwa wajawazito hazipaswi kuwa na vikwazo vya kifedha.
Mtazamo huu unaendana na dhana ya Huduma za Afya kwa Wote, inayosisitiza upatikanaji wa huduma bora, salama na za wakati kwa wote bila kusababisha madhila ya kifedha kwa mtu binafsi au familia.
Wataalamu wa afya ya umma wanaeleza uwepo wa gharama za matibabu huathiri moja kwa moja matumizi na upatikanaji wa huduma muhimu za afya, hususan kwa wajawazito na watoto wachanga.
Ada hizi huwakwamisha wanawake maskini kufika vituo vya afya kwa wakati, jambo linaloongeza uwezekano wa matatizo makubwa ya uzazi, vifo vya mama na vifo vya watoto wachanga, ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuzuilika endapo huduma zingepatikana bila kikwazo cha gharama.
Mtaalamu wa uuguzi na ukunga, Martha Rimoy anasema upo umuhimu kwa wajawazito kupata huduma za afya bure lakini kuangaliwe namna ambayo itawezesha wenye uwezo wajigharamikie na wasio na uwezo wasaidiwe.
Anasema hii ni kwa sababu wajawazito wasio na uwezo kuchangishwa fedha huwaathiri kisaikolojia.
“Gharama ni kikwazo kwa wajawazito katika kupata huduma. Mazingira bora ya kupata huduma yatawawezesha mjamzito kuhudhuria kliniki, kufuatilia chanjo na vipimo muhimu vya afya,”
Martha anasema kwa wanawake wanaoishi katika mazingira duni kiuchumi, mzigo wa gharama za matibabu huwa kikwazo kinachowalazimu kuchelewesha au kuacha kabisa kutafuta huduma za afya kwa wakati unaohitajika kwenye vituo vya kutolea huduma.
Anasema hali hii huongeza hatari ya matatizo ya ujauzito yanayoweza kuzuilika, ikiwemo kutokwa na damu nyingi, shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito na maambukizi, ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia vifo vya mama na watoto wachanga.
Hili linaungwa mkono na Mkurugenzi Mkazi wa Regional Psychosocial Support Initiative (REPPSI), Edwick Mapalala, kuwa mjamzito anapaswa kupata huduma za afya bila kikwazo cha gharama ili kuokoa uhai wa mama na mtoto.
“Watunga sera walipoeleza mjamzito apate matibabu bure waliangalia kulinda uhai wa mtoto na mama, taifa lolote linalolinda uhai wa watu wake maana yake linalinda uchumi,” anasema.
Anasema ni muhimu mjamzito kupata huduma za afya bila kikwazo cha huduma, kwani mjamzito hupitia changamoto nyingi kipindi cha mimba na endapo atakumbana na changamoto zenye kuathiri mwili wake ipo hatari ya kujifungua mtoto mwenye ulemavu.
Hili linafafanuliwa na Dk Daud Emmanuel, kuwa kipindi cha ujauzito na baada ya ujauzito ni kipindi muhimu kwa mama na mtoto kwani afya njema ya wawili hao, na kuwa kina uhusiano na huduma bora za afya alizopata.
“Huduma bora za afya zina matokeo mazuri ya mtoto kuzaliwa na afya njema, mama kubeba ujauzito na kujifungua katika hali nzuri,” amesema.
Mtalamu huyo amesema yapo magonjwa humpata mama akiwa na mtoto tumboni au wakati wa kujifungua mtoto.
Amesema huduma bora za afya huitaji fedha za kupata dawa, kuonana na watalaamu na vipimo vya kubaini maradhi yanayoweza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Kuwa na uhakika wa matibabu kwa mjamzito inasaidia akina mama kuwahi kufika hospitali mapema, kama huduma za afya kwa mama zitakuwa bure mama atakuwa na uwezo wa kuwahi hospitali mapema,” anasema.
Dk Emmanuel anasema mjamzito hupatiwa virutubisho kusaidia damu na kumwepusha mtoto na maradhi, sasa endapo uwezo wa mama haumwezeshi kupata huduma bure za afya, hali hiyo huibua matatizo kwake na mtoto.
Anasema mama anapopitia changamoto ya kupata matibabu kutokana na kipato, upo uwezekano wa kupoteza maisha yeye na mtoto.
“Mama anaweza kuchanika mfuko wa uzazi, mtoto akapata maambukizi ya Ukimwi wakati wa mama kujifungua,” anasema.
“Kikwazo cha fedha humkwamisha mama kuhudhuria kliniki kupata vipimo muhimu, ambavyo vitamsaidia mtaalamu kutambua njia sahihi ya kujifungulia, kama ni kawaida au kwa upasuaji.
“Mama anapokosa uwezo wa kifedha kipindi cha kujifungua anaweza kupata huduma kwa kuchelewa, tofauti na kama hakuna kikwazo cha fedha,” amesema.
Dk Emmanuel anasisistiza huduma za afya kuwa bure, ili akina mama kupata huduma stahiki za afya kumuondolea hatari ya kupoteza maisha.
Uhaba wa bajeti
Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya kijamii na uchumi, Oscar Mkude, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayotaka huduma za matibabu ziwe bure kwa makundi maalumu haijatekelezwa kwa ukamilifu, sababu kubwa ni uhaba wa bajeti.
“Kwa kawaida sera inaweka msingi/malengo ya muda mrefu (matamanio), ambayo yanahitaji mikakati ya rasilmari mbalimbali ili kuitekeleza.
Kwa nchi hizi zetu, kwa kuwa fedha zinakuwa na matumizi mengi, mara nyingi utekelezaji unakuwa hafifu sana.
Mkude amesema demografia ya afya Tanzania 2022 inaonyesha kuwa kiwango cha uzazi kipo juu, wastani ni watoto 3.2 kwa kila mwanamke wa umri wa kuzaa.
Amesema hiyo ina maanisha bajeti ya kuhudumia kundi la mama na mtoto ni lazima iwe kubwa.
Mkude amesema ni muhimu matibabu kwa wajawazito yapatikane bila kikwzo cha fedha kwa lengo la kulinda afya ya jamii, kupunguza umasikini na kufanya huduma ya afya ifikike.
“Unaweza kujenga hospital nyingi lakini watu wakashindwa kuzifikia kwa sababu za kifedha. Hivyo sera inamsingi huo na bado ni muhimu kutekelezwa iwe kwa bima ya afya kwa wote au namna nyingineyo,” amesema.
Mkude amesema kwa muktadha wa afya ya umma, msamaha wa ada za huduma za afya unatambuliwa kimataifa kama nyenzo muhimu katika kupunguza vifo vya akina mama, vinavyosababishwa na uwezo mdogo wa familia zenye kipato cha chini.