
Dar es Salaam. Serikali imeanza kufanya tafiti za upembuzi yakinifu katika miji minne mikubwa nchini ili kuongoza mipango ya baadaye ya miundombinu ya usafiri na kupunguza gharama za fidia kabla ya upanuzi uliopangwa wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka (BRT).
Tafiti hizo zinatarajiwa kutoa msaada wa kitaalamu kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), unaotarajiwa kuwa mamlaka kamili itakayohusika na utekelezaji wa BRT katika miji mbalimbali nchini.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Dart, Saidi Tunda amesema tafiti hizo pia zitasaidia mipango ya muda mrefu ya kuboresha huduma za usafiri wa umma na kudhibiti gharama za uendelezaji wa miundombinu wakati miji ikiendelea kukua.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiandaa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Mijini (UMTA), itakayoipa Dart mamlaka kamili ya kupanua huduma za BRT nje ya Dar es Salaam.
Tunda amesema kwa sasa tafiti hizo zinafanyika katika miji ya Arusha, Mbeya, Mwanza na Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kupanua mifumo ya usafiri wa umma iliyoratibiwa nchini.
Amesema wataalamu wanachunguza namna ya kubaini na kulinda mapema njia za usafiri ili kuepuka madai makubwa ya fidia ambayo mara nyingi huchelewesha utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
“Katika baadhi ya miji kama Dodoma, maeneo ya miundombinu hiyo yalishatengwa tangu hatua za awali za upangaji. Hali hii itapunguza kwa kiasi kikubwa, au hata kuondoa kabisa gharama za fidia,” amesema.
Tunda amebainisha kutenga mapema maeneo ya njia ni miongoni mwa mbinu bora za kudhibiti ongezeko la gharama za upanuzi wa usafiri wa mijini, hasa katika miji inayokuwa kwa kasi ambako makazi holela tayari yamejengwa kwenye maeneo muhimu.
Amesema katika miji yenye msongamano mkubwa wa makazi, tafiti hizo pia zitapendekeza uwezekano wa kutumia mifumo ya usafiri wa chini ya ardhi.
“Ingawa ujenzi wa miundombinu hiyo unahitaji uwekezaji mkubwa mwanzoni, kwa muda mrefu unaweza kuwa nafuu zaidi na kuongeza usalama pamoja na ufanisi wa uendeshaji,” amesema.
Ameongeza njia za chini ya ardhi pia zitalinda miundombinu ya mabasi dhidi ya kuingiliwa na watumiaji wengine wa barabara, wakiwamo waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, wanaoingia kwenye njia maalumu na kuvuruga huduma.
Tunda amesema matumizi ya mchanganyiko wa mifumo ya juu ya ardhi na chini ya ardhi kulingana na jiografia ya kila mji, yataisaidia Tanzania kujenga mfumo imara na wenye ufanisi wa usafiri wa mijini, wakati idadi ya watu ikiendelea kuongezeka kwa kasi.
Aidha, amesema rasimu ya sheria ya UMTA bado inaendelea kuboreshwa ili kuhakikisha inakuwa kamilifu na kuepuka upungufu utakaoweza kuathiri utekelezaji wake baadaye.
Amesema mapitio hayo yanazingatia pia uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa mradi wa BRT Dar es Salaam.
“Tunatarajia sheria hiyo mpya kuwa tayari katika mwaka wa fedha 2026/27, itakayotuwezesha kuanzisha mamlaka kamili na kuanza kupanua huduma katika mikoa mingine,” amesema.
Amesema mfumo huo utakuwa na jukumu muhimu la kuratibu usafiri wa umma mijini, kupunguza msongamano na kurahisisha safari kwa maelfu ya wananchi.
Mtaalamu wa usafiri kutoka Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji (NIT), Prosper Nyaki ameitaka Serikali kuhakikisha tafiti za kina zinafanyika kuhusu usanifu wa vituo vya BRT pamoja na uhalali wa kijamii na kiuchumi kabla ya kupanua mfumo huo katika miji mingine.
Amesema ni muhimu vituo hivyo vikajengwa kwa kuzingatia idadi halisi ya abiria ili kuepuka kujenga miundombinu mikubwa isiyolingana na mahitaji halisi, kama ilivyojitokeza katika baadhi ya vituo Dar es Salaam.
Nyaki amesisitiza umuhimu wa tafiti za kiuchumi kubaini shughuli zitakazochochewa kando ya njia hizo, zikiwamo za viwanda, benki na masoko, pamoja na kutathmini uwezo wa mamlaka za Serikali za mitaa kuendeleza huduma baada ya utekelezaji.
Amesema tathmini za kijamii ni muhimu kubaini jinsi mfumo huo utakavyorahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kama maeneo ya kazi, hospitali na masoko.
“Madhumuni ni kuboresha uhamaji wa watu ili waweze kufikia fursa na huduma muhimu kwa urahisi,” amesema.
Mtaalamu mwingine wa sekta ya usafiri ambaye hakutaka kutajwa jina, ameshauri uteuzi wa maeneo uzingatie ramani sahihi ya maendeleo yaliyopo ili kupunguza athari kwa wananchi na kuepuka gharama zisizo za lazima za fidia.
Amesema utambuzi wa mapema wa mali zitakazoathirika pamoja na ushirikiano wa karibu na mamlaka za mitaa, unaweza kupunguza gharama za fidia na kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara kabla ya kuanzisha mfumo wa BRT, akibainisha kuwa ujenzi wa barabara kuu na za mlisho kwa ubora utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024/25, maelfu ya wananchi walioathiriwa na miradi ya miundombinu bado hawajalipwa fidia yenye thamani ya Sh91.94 bilioni.