Dar es Salaam. Filamu mpya inayosimulia maisha ya marehemu mfalme wa Pop kutoka Marekani, Michael Jackson imeripotiwa kuvunja rekodi ya mapato katika wiki yake ya kwanza ya ufunguzi.

Filamu hiyo iliyopewa jina la ‘Michael’, ambayo imeigizwa na Jaafar Jackson kama muhusika mkuu. Imefanikiwa kuingiza dola 217 milioni duniani kote na kuifanya kuwa filamu ya wasifu (biopic) inayofuatiliwa zaidi.

Kupitia mafanikio hayo, imeivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na ‘Bohemian Rhapsody’, filamu ya mwaka 2018 iliyochezwa na Rami Malek ambapo wiki ya ufunguzi ilifanikiwa kuingiza dola 124 milioni.

Aidha filamu hiyo ya Michael pia imepiku mapato yaliyopatikana katika filamu ya Oppenheimer ambayo iliingiza dola 180 milioni. Hivyo basi Michael imebaki kileleni kuwa filamu ya wasifu iliyopata mapokezi makubwa kimataifa.

Akizungumzia kuhusu mafanikio hayo, mwenyekiti wa kampuni ya Lionsgate, Adam Fogelson, alisema mafanikio hayo yanatokana mwitikio mkubwa kutoka kwa mashabiki wa rika zote.  “Huwezi kufikia kiwango hiki bila kupata mwitikio mkubwa kutoka kila aina ya watu. Watazamaji wanaonekana kufurahia sana,” alisema.

Hatahivyo licha ya mafanikio hayo kwa upande wa watazamaji, filamu hiyo imepokelewa tofauti kwa baadhi ya mashabiki wakidai kuwa filamu imetolewa kwa lengo la kusafisha jina la MJ huku baadhi ya matukio ya unyanyasaji yakiendelea kufichwa.
 
Kwa mujibu wa tovuti ya tathmini za filamu ya ‘Rotten Tomatoes’ filamu hiyo imependwa kwa asilimia 97 huku ikipata ukosoaji kwa asilimia 38.
 
Katika miaka ya hivi karibuni, Hollywood imekuwa ikizalisha kwa wingi filamu za wasifu wa wanamuziki, zikiwemo za Queen, Elton John, Bob Dylan, Aretha Franklin, Elvis Presley, Bruce Springsteen, Bob Marley, Amy Winehouse, kundi la N.W.A, Robbie Williams na Whitney Houston.

Filamu ya Michael imetengenezwa kwa kutumia urithi wa msanii huyo, vilevile baadhi ya vipande hasa alivyokuwa akiimba vilitumia sauti yake halisi. Licha ya kufichwa matukio ya unyanyasaji lakini filamu hiyo imeelezea kwa undani uhusiano wa MJ na baba yake Joseph Jackson, nafasi hiyo ikiigizwa na mwigizaji Colman Domingo.

Kwa mujibu wa taarifa, gharama za utengenezaji wa filamu hiyo ni dola milioni 200. Gharama ambayo imeifanya kuwa moja ya filamu za wasifu (biopic) zilizowahi kutumia mkwanja mrefu Zaidi katika utengenezaji wake.

Aidha ingawa tayari imeanza kuonyeshwa katika nchi nyingi duniani, bado haijafika nchini Japan, ambapo inatarajiwa kuanza kuonyeshwa mwezi Juni.

Mbali na filamu hiyo kuupiga mwingi katika mauzo lakini pia baadhi ya nyimbo zake zimeanza kurudi tena katika chati za muziki illie Jean, Beat It, Smooth Criminal, Black or White, Thriller pamoja na Man in the Mirror, ambapo  zimeripotiwa kuongoze wasikilizaji katika chati za muziki kama Billboard Hot 100, UK Singles Chart na Spotify Global Top 50.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *