Nigeria. Mwigizaji mkongwe nchini Nigeria Chinedu Ikedieze maarufu kama ‘Aki’ amefunguka safari yake ya uigizaji, misoto aliyopitia huku akieleza namna alivyokutana na pacha wake kwenye filamu Osita Iheme ambaye naye anafahamika kama ‘Ukwa’. 

Akizungumza katika Podcast #WithChude ameeleza moja ya matukio muhimu katika maisha yake ni kukutana na pacha wake Osita Iheme. Ambapo walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2001 kipindi ambacho walikuwa wakijitafuta katika tasnia hiyo.

Ameeleza wawili hao hawakuwa marafiki bali walikutana location, ambapo kila mmoja alikuwa akipewa nafasi yake, ameeleza watu waliowaunganisha ni waongozaji wa filamu ambao waligundua kuna Chemistry ya kipekee kati yao hivyo wakaamua kuwapanga pamoja kwenye kazi.

Aidha baada ya kuendelea kupiga kazi pamoja jina la Aki na Pawpaw lilianza kujizolea umaarufu, ambapo Chinedu alieleza kuwa mafanikio yao hayakutokea kwa bahati mbaya bali ni kutokana na mapambano na kuwekeza nguvu katika kazi.

Aligusia kuwa uhusiano wake wa muda mrefu wa kikazi na Osita Iheme. Akieleza urafiki wao umejengwa juu ya heshima na uaminifu wa miaka mingi. Alisisitiza kuwa mafanikio yao kama “Aki na Pawpaw” yamechangiwa sana na kuelewana kazini, kuaminiana na kukua pamoja ndani ya tasnia ya filamu.

Wawili hao walifanikiwa kuwa moja ya duo maarufu nchini Nigeria na duniani kote wakitambulika kupitia kazi zao kama Aki na Ukwa, One Two Brothers, 2 Rat, pamoja na ile waliyoigiza na marehemu Mr Ibu.

Umaarufu wao uliwapelekea kupata fursa mbalimbali kubwa ikiwemo kufanya filamu mfululizo zilizouzwa sana. Mialiko ya kimataifa, na mikataba ya matangazo (endorsements) ya bidhaa tofauti, jambo lililowapa kipato kikubwa na kuwafanya kuwa brand kubwa ya vichekesho kutoka Nollywood.

Licha ya hayo wawili hao wanatajwa kutokuwa na ukaribu kama hapo awali ambapa inaelezwa kuwa kwa sasa kila mmoja ameamua kuendelea na maisha yake binafsi na miradi tofauti ya filamu.

Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo makubwa Chinedu alifunguka namna alivyokumbana na changamoto ya akili iliyotokana na msongo mkubwa wa mawazo.

Alieleza kuwa presha ya maisha ya umaarufu pamoja na mitazamo ya jamii kuhusu umbile lake vilimuweka kwenye kipindi kigumu kilichopelekea msongo mkubwa wa mawazo na afya ya akili.

Aidha Chinedu alikiri kuwa aliwahi kufikiria kujitoa uhai, lakini alifanikiwa kuvuka hali hiyo kutokana na msaada wa familia yake. Alisema hatua kubwa ya uponyaji ilikuwa kuacha kujilinganisha na wengine na kuanza kuthamini maisha yake binafsi bila kujali maoni ya watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *