Dodoma. Takribani Watanzania 60,000 hupata maambukizi mapya ya Ukimwi kila mwaka, huku chanzo kikitajwa kuwa ni ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi.

Kundi la wasichana wanaobalehe, waliovunja ungo na wanawake vijana limetajwa kuwa hatarini zaidi, kwani huathirika mara tatu zaidi ya makundi mengine kutokana na shinikizo la kijamii, tamaa ya mafanikio ya haraka na njia za mkato.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, ametoa kauli hiyo leo Aprili 29, 2026, alipozungumza katika kongamano la vijana lililoandaliwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kuhusu masuala ya Ukimwi na afya ya uzazi.

Profesa Kabudi amesema kinachochangia maambukizi hayo kwa kundi hilo ni ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi, shinikizo la kijamii na tamaa ya mafanikio ya haraka, vinavyochangia baadhi yao kujihusisha na mahusiano hatarishi.

“Rika hili ndio nguvu kazi ya Taifa, na nyakati zinabadilika, hivyo lazima kama Serikali tuweke nguvu katika utoaji wa elimu kwa lengo la kuwasaidia na kuwawezesha mabinti zetu, ili kuwajengea uelewa juu ya masuala haya na kuwakumbusha kuwa hakuna mafanikio bila kutoa jasho,” amesema Profesa Kabudi.

Waziri amesema ili jamii iendelee, inahitaji uimara wa afya ya kundi hili, hivyo ni lazima Serikali ichukue jitihada za haraka katika kukabiliana na tatizo hilo.

Mbali na maambukizi ya Ukimwi, amesema vijana wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili, ambapo asilimia 12 ya vijana wanakumbwa na sonona inayochangiwa na mahusiano na shinikizo la mafanikio.

Amesema takribani asilimia 70 ya vijana hao wanakabiliwa na changamoto ya wasiwasi kutokana na hofu ya kusalitiwa katika mahusiano na kutafuta mafanikio kwa njia za mkato.

Kwa upande wake, mwakilishi wa vijana, Arola Franck, ameiomba Serikali kurahisisha mfumo wa utoaji mikopo kwa vijana, akipendekeza mchakato uanze ngazi ya kata ili kuongeza idadi ya wanufaika.

“Kama vijana tunahitaji kujiendeleza, hivyo tunaomba uwezeshwaji kwenye mitaji, elimu na nafasi za uongozi kwenye maeneo muhimu yatakayotupa nafasi ya kufikisha mawazo yetu kwa urahisi ili yafanyiwe kazi,” amesema Arola.

Mwakilishi wa kundi la vijana wenye ulemavu, Michael Salali, ameomba kuwekwa kwa utaratibu wa utoaji wa mafunzo ya lugha ya alama kwa watoa huduma za afya nchini ili kuwajengea uwezo wa mawasiliano na watu wenye ulemavu wa kusikia wanapopata huduma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *