
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limewapitisha mbunge wa zamani wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale na Said Miraji Abdulla kuwa manaibu makatibu wakuu wa chama hicho, Tanzania Bara na Zanzibar.
Mbali na hilo, baraza hilo lililoketi jana Jumanne Aprili 28, 2026 limewapitisha pia wakurugenzi 14 wa idara mbalimbali za chama hicho.
Kati ya wakurugenzi hao, watatu ndio waliobaki kutoka katika uongozi uliopita wa Profesa Ibrahim Lipumba, wakati 11 ni maingizo mapya.
Kwa hatua hiyo, CUF inajaza nafasi zilizokuwa wazi tangu Februari 2026, baada ya Mirambo Yusuph kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, akichukua nafasi ya Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba aliyedumu uenyekiti kwa miaka 27 aliondolewa madarakani Februari 14, 2026, baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uchaguzi uliomweka madarakani yeye na wenzake watano.
Mbali na Profesa Lipumba, wengine walioathirika na uamuzi huo ni makamu wenyeviti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya (Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mohamed Ngulangwa ameliambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 29, 2026 kikao cha baraza kuu hilo kilifanyika ofisi za makuu ya chama hicho Buguruni.
“Lengo kubwa la kikao cha jana ni kukamilisha safu za uongozi baada matukio yaliyotokea. Nafasi zilizojazwa jana ni pamoja za wakurugenzi na manaibu makatibu wakuu,” amesema Ngulangwa.
Katika orodha hiyo waliorejea tena ni pamoja na Mohamed Ngulangwa (Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma), Zainab Mndolwa (Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi) na Ali Rashid Abarani (Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma).
Ingizo jipya ni Mohamed Zuberi (Naibu Mkurugenzi wa Itifaki na Udhibiti) Abdallah Dadi Ubwa (Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge/Uwakilishi, Sera na Utafiti), Anna Paul (Naibu Mkurugenzi Mambo ya Nje, Bunge/ Uwakilishi, Sera na Utafiti) na Masoud Mhina (Mkurugenzi Siasa na Matukio).
Wengine ni Ali Makame Issa (Naibu Mkurugenzi Siasa na Matukio), Hamad Mmanga maarufu Master (Mkurugenzi wa Itifaki na Udhibiti), Dauda Hassan (Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria), Nassoro Masusi (Naibu Mkurugenzi Haki za Binadamu na Sheria).
Pia, wamo Mwadini Jecha (Naibu Mkurugenzi Mipango na Uchaguzi), Attiye Magram (Naibu Mkurugenzi Fedha na Uchumi) na Juma Nkumbi (Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi).