
Arusha. Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-Tan), Edwin Soko, amesema hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini si nzuri, akieleza kuwa ni muhimu kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoundwa na Serikali na kuongozwa na Tido Mhando, Januari 24, 2023.
Soko amesema hayo leo, Jumatano Aprili 29, 2026, katika maadhimisho yanayoendelea ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD 2026), yatakayofikia kilele Mei 3, 2026.
Amesema hadi sasa wanahabari wengi wanafanya kazi katika mazingira duni, huku vyombo vya habari vikikosa vyanzo vya kutosha vya mapato, kuchelewa kwa mishahara na kukosa bima ya afya.
Amesema utekelezaji wa mapendekezo ya kamati hiyo, ambayo yalikabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, utaweza kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kutathmini mustakabali wa vyombo vya habari, hasa changamoto ya kupungua kwa mapato pamoja na mabadiliko ya teknolojia.
Balile amesema bado kuna wasiwasi kuhusu mwenendo wa Serikali kutunga au kutorekebisha sheria zinazodaiwa kukwamisha uhuru wa vyombo vya habari.
Ameeleza kuwa vyombo vya habari vinapokuwa huru kiuchumi, vinaweza kutekeleza majukumu yake bila hofu ya kukosa matangazo kutoka serikalini au sekta binafsi, pamoja na kuepuka hatari ya kufungiwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa vyombo hivyo kuwa na uwezo wa kufikia maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kupata taarifa sahihi kwa umma.
Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema hali ya uhuru wa habari nchini imeendelea kudorora kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza, pamoja na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari na kutotekelezwa kwa amri za mahakama kuhusu marekebisho ya sheria kandamizi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, amesema mwaka 2025 uliokuwa na mchakato wa uchaguzi mkuu uliambatana na matukio yaliyoathiri moja kwa moja wanahabari, ikiwemo kukamatwa na kunyang’anywa vitendea kazi.
Dk Henga amesema takribani wanahabari wasiopungua wanane walikamatwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mara na Arusha, huku baadhi yao wakishikiliwa bila kufikishwa mahakamani, hali inayotishia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kujieleza.
Amesema kuporomoka kwa uhuru wa vyombo vya habari kulionekana zaidi mwaka jana kutokana na mazingira ya uchaguzi, na kulishuhudiwa matukio ya wanahabari kupotea, kuchukuliwa hatua na vyombo vya habari kufungiwa.
Kwa mujibu wa LHRC, katika kipindi cha uchaguzi na baada yake, kulirekodiwa matukio nane ya kukamatwa kwa wanahabari kinyume cha sheria, pamoja na matukio ya kupotea kwa baadhi yao na kufungwa kwa huduma za intaneti, jambo lililoathiri utendaji kazi wa vyombo vya habari mtandaoni.
Aidha, kituo hicho kimeeleza kuwa vyombo kadhaa vilifungiwa mwaka jana, vikiwemo Jamii Media kwa siku 90, pamoja na Baraka FM, Ayo TV na Nyota TV, hatua ambayo imetajwa kutokidhi matarajio ya kukuza uhuru wa kujieleza nchini.
Dk Henga ameongeza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kumerekodiwa matukio manane ya wanahabari au vyombo vya habari kuchukuliwa hatua, akimtaja mwanahabari Aloyce Nyanda aliyekamatwa na baadaye kuachiwa kutoka na shinikizo la wanaharakati.
Pia ametaja kufungiwa kwa Jambo TV kwa siku 90, akisisitiza kuwa hali ya uhuru wa vyombo vya habari bado si ya kuridhisha.