
Dar es Salaam. Kampuni ya X (zamani Twitter) imetimiza moja ya ahadi zake kuu za kimkakati kwa kuzindua programu mpya ya ujumbe mfupi inayojulikana kama ‘XChat’, hatua inayotajwa kuashiria ushindani mkali dhidi ya majukwaa makubwa kama WhatsApp na Telegram.
Uzinduzi huu, ambao umefanyika Aprili 24, 2026 kwa watumiami wa iOS, ni sehemu ya mpango kabambe wa mmiliki wa kampuni hiyo, Elon Musk, wa kuigeuza X kuwa “Everything App” (programu ya kila kitu), ikijumuisha mawasiliano ya kijamii, huduma za fedha, na sasa ujumbe wa faragha.
XChat innalenga kuingia moja kwa moja katika ushindani na programu kubwa za ujumbe (messaging apps) zilizojichimbia mizizi duniani kwani mkakati wa bilionea Musk ni kuifanya XChat kuwa mbadala wa programu hizo kwa kuweka msisitizo kwenye faragha (privacy) na muunganiko na mtandao wa X.
Ukianza na programu kuu kama WhatsApp ambayo hadi kufikia mapema mwaka huu wa 2026 ina zaidi ya watumiaji bilioni 3.3 wanaotumia kila mwezi huku ikiendelea kukua kwa kasi, na inatarajiwa kufikia watumiaji bilioni 3.5 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
WhatsApp ndiyo programu inayotumiwa zaidi duniani. XChat inalenga kuvuta watumiaji wa WhatsApp kwa kuwapa jukwaa ambalo halina matangazo na linalojitenga na mfumo wa kampuni ya Meta.
Wakati WhatsApp inahitaji namba ya simu kusajili, XChat inatumia akaunti yako ya X (Twitter), jambo linaloweza kuvutia watu wanaotaka mawasiliano bila kutoa namba zao za simu binafsi.
Upande wa Telegram ni maarufu kwa makundi makubwa ya jumuiya za watu, hususan katika sekta ya teknolojia, siasa, na fedha za kidijitali hapa XChat inalenga kuchukua nafasi hiyo kwa kuruhusu makundi makubwa na kutoa mazingira ya “kijamii” zaidi kwa wale wanaotumia X kwa habari na mijadala, huku ikiahidi usalama wa juu zaidi (end-to-end encryption).
Upande wa Signal yenye ubora wa juu katiaka usalama na faragha hapa XChat inajaribu kushindana kwa kutumia teknolojia ya end-to-end encryption ili kujenga uaminifu kwa watumiaji wanaojali sana taarifa zao.
Mawasiliano ya zamani X
Tofauti na mfumo wa awali wa ujumbe wa moja kwa moja (DM) uliokuwepo ndani ya X, XChat inakuja kama programu inayojitegemea ambayo imejikita zaidi katika usalama wa mtumiaji.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa watengenezaji wa programu hiyo, XChat inatumia teknolojia ya kisasa ya End-to-End Encryption.
Hii ina maana kuwa ujumbe, picha, na video zinazotumwa kupitia programu hii zinalindwa kiasi kwamba ni mtumaji na mpokeaji pekee ndio wenye funguo za kusoma maudhui hayo.
Hata kampuni ya X yenyewe haina uwezo wa kuona au kusoma mawasiliano hayo, jambo ambalo ni kigezo kikubwa kwa watumiaji wanaojali faragha (privacy).
Sifa za XChat
Katika XChat kunazuio la ‘screenshot’ kupitia teknolojia ya kuzuia mtumiaji mwingine kupiga picha ya skrini ya mazungumzo bila idhini, jambo linaloongeza usalama wa taarifa nyeti.
Ujumbe wa Muda (Disappearing Messages) ambapo mutumiaji ana uwezo wa kuweka muda wa ujumbe kujifuta wenyewe, kuanzia sekunde hadi saa kadhaa.
Pia upo uhuru wa Kuhariri ukiwa ni uwezo wa kuhariri ujumbe hata baada ya kuutuma umewezeshwa kwa watumiaji wote, ukiwa na alama ya “Edited” ili kuonyesha mabadiliko yamefanyika.
XChat imeunganushwa na X, ambapo inatumia mfumo wa akaunti moja (Single Sign-On), ikimaanisha watumiaji wanaweza kuingia kwa kutumia taarifa zao za kawaida za X bila kuhitaji usajili mpya.
Kibiashara zaidi
Uzinduzi wa XChat unatazamwa pia kama hatua ya kibiashara. Kwa kuweka miundombinu imara ya mawasiliano, X inajiandaa kuanzisha huduma za malipo (X Payments) ambazo zinatarajiwa kuruhusu watumiaji kutumiana pesa moja kwa moja kupitia programu hiyo.
Huku soko la teknolojia likizidi kubadilika, XChat inaonekana kuwa kete muhimu ya Elon Musk katika vita dhidi ya makubwa ya teknolojia (Big Tech) duniani.
Taarifa zaidi zinaeleza XChat imeanza kupatikana kwa watumiaji wa vifaa vya iOS pekee, huku watumiaji wa Android wakitarajiwa kusubiri hadi matangazo rasmi yatakapotolewa.