Arusha. Serikali imesema haina mpango wa kusimamisha au kuzuia shughuli za uwindaji wa kitalii nchini, badala yake itaendelea kuuboresha ili kukuza mchango wake katika uchumi na kuongeza Pato la Taifa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Aprili 29, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas, wakati akizungumza katika kikao kazi cha wadau wa uwindaji wa kitalii nchini kinachofanyika jijini Arusha.

Dk Abbas amesema Serikali itaendelea kuandaa na kuboresha sera zitakazohakikisha shughuli za uwindaji wa kitalii zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi wa wanyamapori, sambamba na kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya uwindaji.

Amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa tasnia hiyo ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, katika kukuza uchumi wa Taifa, kuhifadhi mazingira na kuboresha ustawi wa jamii, hivyo haina nia ya kuisimamisha.

“Nafahamu zipo changamoto kadhaa, ikiwemo mjadala wa VAT na masuala mengine, lakini Serikali itaendelea kuwahakikishia kuwa sera ya uwindaji wa kitalii ipo imara na itaendelea kutekelezwa,” amesema Dk Abbas.

Amesema hakuna uwindaji uliosimamishwa nchini wala mpango wa kuusimamisha huku  akisisitiza maboresho ya sekta hiyo yataendelea kufanyika ili kuimarisha ufanisi wake.

Kwa mujibu wa Dk Abbas, kikao kazi hicho kinafanyika katika kipindi ambacho sekta ya utalii nchini inayotegemea rasilimali za wanyamapori, inachangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, rasmi na zisizo rasmi.

Amesema ndani ya sekta hiyo, uwindaji wa kitalii ni miongoni mwa maeneo yanayochangia mapato makubwa licha ya kuvutia idadi ndogo ya watalii.

“Takwimu zinaonyesha kwa mwaka, Tanzania hupokea wastani wa watalii 448 wa uwindaji, wanaoingiza zaidi ya Sh41.7 bilioni. Hii inaonesha licha ya idadi yao kuwa ndogo ukilinganisha na watalii wa picha, mchango wao kifedha ni mkubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuongeza idadi ya watalii wa uwindaji wa kitalii hadi kufikia 1,500 kwa mwaka na kuongeza mapato hadi kufikia Sh100 bilioni.

Aidha, amesema kwa wastani Bara la Afrika hupoteza takribani watalii 20,000 wa uwindaji kila mwaka, wanaoweza kuingiza zaidi ya dola za Marekani milioni 200, akisisitiza umuhimu wa Tanzania kutumia fursa hiyo ipasavyo.

Hivyo, Dk Abbas amewataka wadau wa sekta hiyo kuilinda kwa kuzingatia maadili ya kazi, kuheshimu masharti ya uwindaji, kushiriki katika juhudi za kupambana na ujangili pamoja na kulipa kodi na stahiki za jamii zinazozunguka maeneo ya uwindaji.

“Tunawathamini sana wadau na wawekezaji wetu. Ni wajibu wetu sote kulinda sekta hii kwa kuweka maadili mbele na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka wizara hiyo, Dk Alexander Lobora amesema idara hiyo huandaa mikutano ya wadau wa uwindaji wa kitalii kila mwaka ili kujadili hali ya sekta, changamoto zake na kuweka mikakati ya kuboresha.

Amesema mikutano hiyo imekuwa na manufaa makubwa, akitolea mfano kupatikana kwa suluhisho la changamoto ya ongezeko la bei ya vitalu na ada za wanyamapori ya mwaka 2007, pamoja na mafanikio katika kudhibiti ujangili wa tembo na biashara haramu ya nyara kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa ‘Elephant Ivory Action Plan.’

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji Tanzania (Tahoa), Michel Mantheakis amesema chama hicho kitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Naye mdau wa uwindaji wa kitalii na mwindaji bingwa, Paul Horsley, amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ujangili ili kulinda rasilimali za wanyamapori.

“Tumeweka doria katika maeneo ya uwindaji ili kuhakikisha wanyamapori wanalindwa. Serikali imetupa moyo kwa kutambua changamoto zinazokabili sekta hii na imetuhakikishia kuwa hakuna mpango wa kusimamisha uwindaji wa kitalii,” amesema.

Ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni pamoja na tozo na kodi, akieleza matumaini kuwa kupitia majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali na wadau, suluhisho litapatikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *