SIMBA ndiyo bingwa mpya wa Kombe la Muungano baada ya kufanya kweli ikiivua ubingwa huo mtani wake wa jadi, Yanga kwenye fainali kali iliyopigwa Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ubingwa huo haukuwa mwepesi kwani Simba ililazimika kutumia dakika 120 kujihakikishia mafanikio hayo ya kwanza msimu huu, baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa hazijafungana na kuongezwa zingine 30 na Wekundu hao wa Msimbazi kupata bao dakika ya 118 kwa penalti ya mshambuliaji, Seleman Mwalimu.

SIMBA 04

SIMBA INAENDELEA

Simba ni kama inaendelea kuipelekea Yanga ujumbe, zama zimebadilika na Wekundu hao wanataka kurudisha heshima yao kwenye mbio za mataji na baada ya mechi ya kwanza ambayo ni ya ligi kumalizika kwa suluhu, juzi ikaenda kutengeneza ushindi huo ndani ya dakika 120.

Ushindi huo kwa Simba ni wa kwanza dhidi ya Yanga tangu ishinde mara ya mwisho Agosti 13, 2023 kwenye Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1.

Baada ya hapo, Yanga ikashinda mechi sita mfululizo zikiwemo nne za Ligi Kuu Bara na mbili za Ngao ya Jamii, kisha ile ya saba ikawa 0-0, kabla ya Simba kushinda juzi. 

SIMBA 07

PACHA YA RUSHINE, TOURE

Ukuta wa Simba umeimarika, kazi kubwa ikifanywa na mabeki wawili wa kati waliosajiliwa vipindi viwili tofauti msimu huu, Rushine De Reuck na Ismael Toure ambao wamekuwa tishio kuzima mashambulizi yote makali ya Yanga.

SIMBA 08

Mabeki hao wameifanya Simba kumaliza michuano hii bila ya kuruhusu bao baada ya timu hiyo kucheza mechi tatu ikianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mafunzo, kisha 3-0 mbele ya Mlandege na kumaliza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

OURA MAPEMA TU

Winga Anicet Oura ni ubishi wake tu kutaka kuisaidia Simba, lakini mapema kabisa dakika tatu za kwanza zilitosha kucheza dabi hiyo ya pili kwake, baada ya kuumia nyama za paja na kuanzia hapo alishindwa kufanya mambo yake na kugeuka mzururaji uwanjani.

Kocha wa Simba, Steve Barker alifanya uamuzi mgumu akimtoa dakika ya 26 baada ya kuona ni kama timu inacheza pungufu kwa upande mmoja na kupungua kasi ya kutengeneza mashambulizi, hivyo kumwingiza Mwalimu ambaye aliongeza mashambulizi hatari langoni mwa Yanga.

SIMBA 09

YAO AMERUDI

Beki wa kulia wa Yanga, Yao Kouassi alirejea kwenye dabi kwa mara ya kwanza akianza na kuonyesha kiwango bora eneo hilo akikaba kwa nguvu na kupandisha mashambulizi.

Yao alikuwa na hesabu nzuri kwa upande ambao alianza kukabana na Oura, baadaye akaja Clatous Chama na kuifanya Yanga kutulia tofauti na mchezo uliopita na Simba ilitengeneza mashambulizi mengi kutokea pembeni.

SIMBA 11

OKELLO, PACOME WALIPOTEA

Yanga ilitegemea ubunifu wa viungo wake wawili kwenye mchezo huo, Pacome Zouzoua na Allan Okello lakini bahati mbaya hesabu zao nyingi hazikuwa kubwa kuitingisha Simba na kukamatika kirahisi.

Pacome hakuwa kwenye kiwango bora kama ilivyotarajiwa na wakati mwingi mikimbio yake iliipunguza nguvu Yanga, pia alishindwa kufanya maamuzi ya kutoa pasi za haraka ili timu iende na kujikuta akikwama mbele ya viungo na mabeki wa Simba.

Okello hesabu zake nyingi za pasi na mashuti hazikuwa na hatari ya kuilazimisha Simba kufanya makosa na kila alipojaribu kukimbia na mpira, alikabiliana na Toure au Rushine.

SIMBA 12

Hata hivyo, katika safu ya ushambuliaji, ni Prince Dube pekee aliyeonyesha kuwa na kasi kubwa ya kutengeneza mashambulizi na kulazimika kukimbia kwa muda mwingi na kumsababishia maumivu ya nyonga mwishoni mwa mchezo.

SIMBA 03

KAPOMBE ALIAMUA

Baada ya Simba kupata penalti, kuna tukio lilijiri ambalo inawezekana wengi hawakuliona la beki Shomari Kapombe kufanya uamuzi mgumu wa kumchagua Mwalimu kwenda kupiga penalti badala ya Neo Maema na Chama ambao walitaka kufanya hivyo.

Kapombe ambaye ni nahodha wa Simba, alionekana kumsisitiza jambo Mwalimu na kweli mshambuliaji huyo akaenda kupiga penalti nzuri iliyokwenda kufuta kiu ya mataji kwa Wekundu hao.

SIMBA 01

YANGA WALISHTUKA

Kabla ya Mwalimu kwenda kupiga penalti hiyo, kuna tukio lingine liliendelea kwa Yanga na baada ya Maema na Chama kuonekana wanataka kwenda kupiga, makocha wa Yanga walimuita kiungo Aziz Andabwile kumpelekea kipa Djigui Diarra uchaguzi wa wapi wawili hao penalti zao zinakwenda lakini bahati mbaya muuaji akawa mwingine.

DABI MEI 3

Mchezo huo ulionekana kuathiriwa na hesabu za dabi ya ligi itakayopigwa Mei 3, mwaka huu, Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo, jijini Dar es Salaam na timu zote zilionekana kugoma kujiachia sana ingawa kadiri muda ulivyosogea ziliendelea kutafuta ushindi kwa kusambuliana kwa nguvu.

Nguvu ambayo wachezaji wote wamezitumia kwenye mchezo wa juzi ni wazi zitapunguza kasi na ubunifu kwenye mchezo baina ya timu hizo wikiendi hii kutokana na namna walivyotumia nguvu kwenye mchezo wa fainali ya Muungano.

Mabenchi yote ya ufundi yatakuwa na kazi kubwa ya kurudisha utimamu wa miili ya wachezaji hao endapo wanataka kuna timu hizo zinafanya vizuri kwenye mchezo huo uliobeba sura ya nani anaweza kwenda kujitengenezea njia ya kuchukua ubingwa wa ligi.

SIMBA 10

PEDRO BADO ANASUBIRI

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves bado hajaonyesha ubora wake tofauti na wenzake waliotangulia katika kushinda mechi za dabi dhidi ya Simba na juzi alipoteza mechi ya kwanza wakati mwenzake wa Simba Steve Barker akionja ladha ya ushindi.

Kabla ya Pedro, alipita Miguel Gamondi ambaye alikuwa kocha wa mwisho kufungwa na Simba katika Ngao ya Jamii 2023. Baada ya hapo, kocha huyo Muargentina akaichapa Simba mara nne ikiwemo kipigo kizito cha 5-1, kisha Miloud Hamdi akashinda moja katika ligi sawa na Romain Folz aliyefanya hivyo katika Ngao ya Jamii.

Alipokuja Pedro, alianza na matokeo ya 0-0 katika ligi, kisha akapokea kipigo cha 1-0 ambacho kilihitimisha matokeo mazuri ya Yanga mbele ya Simba.

SIMBA 02

TUZO ZOTE SIMBA

Baada ya mechi ya fainali, Simba iliondoka uwanjani na tuzo zote na ukiweka kando kombe sambamba na fedha Sh150 milioni za bingwa, pia ikatoa Mchezaji Bora (Rushine De Reuck), Kocha Bora (Steve Barker), Mfungaji Bora (Seleman Mwalimu), Kipa Bora (Hussein Abel) na Mchezaji Chipukizi (Hussein Mbegu).

Hata hivyo, gumzo lilikuwa kwa upande wa Tuzo ya Mfungaji Bora na Mwalimu licha ya kulingana mabao na Prince Dube wa Yanga kila mmoja akifunga matatu, lakini mshambuliaji huyo wa Simba alikabidhiwa peke yake.

Wengi waliona kama waandaji walitakiwa kuwapa washambuliaji hao wawili kila mmoja tuzo yake baada ya kulingana kwa kila mmoja kufikisha mabao matatu katika mashindano hayo.

MWAMUZI SAFI

Mwamuzi wa kati, Dickens Mimisa Nyagrowa raia Kenya, alifanya kazi yake nzuri kiasi cha wengi kumpongeza kutokana na matukio mengi kuyaamua inavyopaswa.

Kubwa zaidi ni kitendo cha kufika kwenye matukio kwa wakati, huku pia akiwaonya wachezaji mara kwa mara kwa mdomo akiwa sio mtu wa kutoa sana kadi. Alionyesha kadi moja tu kwa Prince Dube.

Lakini kitendo cha kuamua mkwaju wa penalti dakika za mwishoni kabisa, imetajwa kama ujasiri wake mkubwa alioufanya katika mchezo huo kwani waamuzi wengi wakati kama ule, hutumia busara kufanya uamuzi na sio kusimamia sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *