Mbeya. Vikundi 31 vya wanawake, vijana na watu wenye walemavu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya vimenufaika na mikopo wa zaidi ya Sh 721.8 milioni.
Mikopo hiyo imetolewa kama sehemu ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo ikiwa ni kutekeleza maelekezo ya Serikali kuwezesha wananchi kiuchumi.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justine Kijazi leo Alhamisi Aprili 30, 2026 wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Tatu ya kilichofanyika katika Ukumbi wa Meya.
Kijaji amesema kati ya vikundi 31, vikundi vya wanawake 14, vimepata mkopo wa Sh261 milioni, huku vya vijana vikiwa 11, vimekopeshwa Sh435, sambamba na vikundi sita vya watu wenye ulemavu Sh25 milioni.
Kijazi amesema katika kipindi hicho kiasi cha Sh395 milioni, sawa na asilimia 82 ya malengo zimerejeshwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka.
“Changamoto kubwa katika masuala ya utoaji ni wingi wa maombi ya vikundi ukilinganisha na fedha zilizopo,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Mbeya,Justine Kijazi akitoa taarifa kwenye kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Alhamisi Aprili 30,2026. Picha na Hawa Mathias
Mipango miji
Kajazi amesema katika robo ya tatu divisheni ya ardhi imepata zaidi ya Sh111 milioni, kwa ajili ya kazi ya mradi wa viwanja vya Nsalaga na kuandaa mawe mipaka, uthamini mali za wananchi na kuandaa michoro ya mipango miji miwili.
“Divisheni ya mipango miji na ardhi bado inaendelea kushughulikia, lakini mafanikio ni pamoja na kuandaa hati 658, hususani maeneo ya viwanja yaliyo pimwa ikiwepo Nsalaga, Mwansekwa, Mbeya Peack na Iduda,”amesema.
Mstahiki Meya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema hatua ya halmashauri hiyo kupata hati safi inatokana na ushirikiano katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema halmashauri hiyo imevuka malengo kwa kutenga asilimia 70 ya mapato ya ndani kuelekea kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Issa amesema katika robo ya tatu wametumia Sh8 bilioni kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu na afya.
“Taarifa CAG, Halmashauri tumepata hati safi, lakini nisisitize madiwani kama kuna fedha zimefika kwa ajili ya kutekeleza miradi simamieni na siyo kufika mwisho wa mwaka wa fedha zinarudi Serikali,” amesema.
Katika hatua nyingine, Issa amesema halmashauri itatoa vishikwambi kwa madiwani wote kata 36 ili kuwawezesha kupitia taarifa za vikao kabla.
Baadhi ya madiwani Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Uyole wakifuatilia taarifa mbalimbali katika kikao cha robo cha Baraza la Madiwani katika Ukumbi wa Meya .Picha na Hawa Mathias
Kuhusu kilio ubovu wa barabara
Issa amemuagiza Mhandisi wa Jiji, Yunus Nsegobya kuhakikisha anakuwa mkali kusimamia makandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara zinazo tekelezwa kupitia mradi wa Tactics kukamilika kwa wakati.
Issa amesema katika kuhakikisha wanatatua changamoto za barabara za mitaa, halmashauri imetumia Sh500 milioni kununua mtambo wa kuchonga barabara.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa kutoka Ofisi ya Serikali za Mitaa, Edward Malima ameipongeza halmashauri hiyo kufanya vizuri na kupata hati safi hususani kushika nafasi ya tatu kwa ukusanyaji wa mapato asilimia 91.
“Ongezeko ukusanyaji wa mapato,lakini pia ombeni Serikali kuongezewa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha kwani uwezo mnao sambamba na kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali znakamilisha miradi na sio kufika Juni zinarejeshwa,” amesema.
Kauli za madiwani
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mwasanga, Brandy Nelson amesema hatua ya halmashauri kutoa mikopo kwa vijana kumwezesha kuondoa vijana tegemezi kwenye jamii.
“Tunaona vijana wengi wako bize kujitafutia baada ya kupata mikopo asilimia 10, lakini kwa upande wa miradi fedha zinafika kwa wakati na miradi inatekelezwa kwa ubora,” amesema.