
Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewataka wakuu wa polisi wa wilaya, waratibu wa Polisi Jamii wa mkoa na wilaya, wakuu wa vituo pamoja na Polisi Kata kutoka maofisini na kwenda kushirikiana na wananchi katika kuzuia na kutatua changamoto za kiusalama.
Ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Aprili 30, 2026, wakati wa Baraza la Kamanda wa Polisi Mkoa lililowakutanisha maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Mabatini, Wilaya ya Nyamagana.
Akizungumza katika baraza hilo, Mutafungwa amesema maofisa na Polisi Kata wanapaswa kuwa karibu na wananchi kwa kufanya mikutano ya mara kwa mara, kusikiliza kero zao na kushirikiana nao kutatua changamoto kabla hazijageuka matukio ya uhalifu.
“Wakaguzi wa kata, hamieni kwenye kata zenu. Kila mkaguzi aende kwenye kata aliyopangiwa na Afande IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) na atimize wajibu wake wa kukutana na wananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa askari kwenda katika makundi mbalimbali ya kijamii, kutambua migogoro ya kifamilia, ardhi na kijamii, na kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali kuitatua mapema ili kuzuia uhalifu.
“Viongozi wetu wamekuwa wakisisitiza tutoke maofisini tukazungumze na wananchi. Ninarudia tena kuwataka mfanye hivyo kwa vitendo,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Polisi Kata wa Mabatini, Shabani Kashakara, ameahidi kutekeleza maelekezo hayo, huku akiwahimiza Polisi Kata wengine ambao bado hawajafika katika maeneo yao kufanya hivyo mara moja.
Naye Fatuma Mpinga, Polisi Kata wa Mirongo, amewataka wananchi kuacha uoga na kufika katika ofisi za watendaji wa kata ili kuwasilisha changamoto zao za kiusalama, akibainisha kuwa uoga unaweza kuchangia baadhi ya watu kuingia kwenye vitendo vya uhalifu bila kujua.
Aidha, Musa Jilatu wa Kata ya Kishiri ameahidi kutoa huduma bora na ya karibu kwa wananchi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.
Wakati huohuo, Koplo Stella Lyimo wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana amemkabidhi Mutafungwa tuzo na vyeti alivyopokea Aprili 25, 2026, kwa kutambua mchango wake katika ustawi wa jamii.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuthamini askari wanaofanya kazi kwa bidii na weledi, huku akiwahimiza wengine kuongeza juhudi na nidhamu kazini.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka, Koplo Stella ameonyesha umahiri mkubwa katika kutoa elimu kwa jamii, hali iliyosaidia kuleta mabadiliko chanya na kupunguza vitendo vya ukatili.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo, Koplo Stella amesema mafanikio yake yametokana na ushirikiano mzuri kati yake, Jeshi la Polisi na jamii.
“Tuzo hii ni chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha jamii inaendelea kuamini na kushirikiana na Jeshi la Polisi,” amesema.