
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekataa ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, la kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali ndani ya chama hicho kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikisema hajaonyesha kuwa na masilahi ya moja kwa moja katika shauri hilo.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, kwa kushirikiana na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu). Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Lissu aliomba kuunganishwa kama mdaiwa wa lazima, akidai kuwa ana masilahi makubwa kutokana na nafasi yake ya uenyekiti, na kwamba uamuzi wowote wa mahakama utamuathiri moja kwa moja.
Awali, wadai wa kesi ya msingi waliwasilisha pingamizi wakitaka maombi hayo yatupiliwe mbali kwa madai ya kasoro za kisheria. Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupiliwa mbali na mahakama na kumpa Lissu fursa ya kusikilizwa.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama kupitia uamuzi uliotolewa na Jaji Hamidu Mwanga na kusomwa leo Aprili 30, 2026 na Naibu Msajili, Hussein Mushi, imekataa ombi hilo. Mahakama imesema Lissu hajaonyesha masilahi ya karibu yanayompa sifa ya kuunganishwa katika kesi hiyo kwa jina lake binafsi.
Katika uamuzi huo, Jaji Mwanga amebainisha kuwa masilahi aliyoyawasilisha Lissu ni ya kiuwakilishi kutokana na nafasi yake ya uenyekiti, na si ya moja kwa moja. Aidha, imeelezwa kuwa nafasi hiyo inaweza kushikiliwa na mtu yeyote wakati wowote, hivyo haiwezi kuwa msingi wa mahakama kutumia mamlaka yake chini ya Amri ya 1, Kanuni ya 10(2) ya Sheria ya Mashauri ya Madai (CPC) kumjumuisha katika shauri hilo.
“Kwa sababu hiyo maombi haya hayana mashiko na ninayatupilia mbali,” amenukuliwa Naibu Msajili Mushi akirejea uamuzi wa Jaji Mwanga.
Hoja za Lissu
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Lissu alisisitiza kuwa yeye ni mhusika muhimu katika kesi hiyo kwa kuwa ndiye mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, nafasi aliyoshinda kupitia uchaguzi wa ndani wa chama uliofanyika Januari 21, 2025.
Alieleza kuwa ni mwanachama wa Chadema tangu Julai 2004, akiwa na uzoefu wa takribani miaka 21 ndani ya chama hicho, ambapo amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu ikiwemo Mkurugenzi wa Sheria, Mwanasheria Mkuu wa chama, na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara. Pia amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu tangu alipojiunga na chama.
Lissu alidai kuwa uzoefu huo unampa uelewa mpana wa masuala yote makubwa ya chama, ikiwemo sera, maamuzi ya vikao na masuala ya Muungano pamoja na Zanzibar.
Aliongeza kuwa, kama mwenyekiti wa chama Taifa, yeye ndiye anayeongoza vikao vyote vya juu vya maamuzi, ikiwemo Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa.
Kwa mujibu wake, shauri la msingi linahusu masuala hayo hayo ya sera, maamuzi ya chama na hata uongozi wake moja kwa moja, kwani lilifunguliwa muda mfupi baada ya yeye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti na siku chache baada ya kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uhaini.
Lissu alisisitiza kuwa utekelezaji wa uamuzi wowote wa Mmahakama kwenye shauri hilo utakuwa chini ya uongozi wake, hivyo utamuathiri moja kwa moja.
“Mheshimiwa Jaji, amri yoyote utakayotoa, ikiwemo kusimamisha shughuli za chama, itamaanisha mwenyekiti hatoweza kuongoza vikao vya chama ikiwemo mkutano mkuu,” alinukuliwa akisema.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Amri ya I, Kanuni ya II ya Sheria ya Mashauri ya Madai, mahakama ilipaswa kumjumuisha mwenyekiti katika kesi hiyo kama mdaiwa wa lazima.
Majibu ya walalamikaji
Wakijibu hoja hizo, mawakili Shaban Marijan na Alvin Fidelis waliowawakilisha walalamikaji, walipinga ombi hilo, wakidai kuwa Lissu hana sifa za kuunganishwa katika kesi hiyo.
Walisema kuwa Lissu aliwasilisha maombi yake kama mtu binafsi badala ya kutumia nafasi yake ya uenyekiti, jambo linalomkosesha masilahi ya moja kwa moja katika shauri hilo.
Pia walipinga hoja kwamba kesi hiyo imefunguliwa kutokana na uenyekiti wake, wakieleza kuwa madai yaliyopo yanahusu matukio ya muda mrefu tangu mwaka 2016.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kuwa kuna mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya Chadema.
Kwa sasa, kesi hiyo imehamishwa kutoka kwa Jaji Mwanga kufuatia amri ya Mahakama ya Rufani iliyoondoa zuio la muda la Chadema kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama, lililokuwa limetolewa na Jaji Mwanga; na sasa itasikilizwa na Jaji David Ngunyale.