
Dar es Salaam. Ni hatua nzuri, ndivyo unavyoweza kusema ukizungumzia mazungumzo ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar kati ya ACT- Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) ikielezwa yapo katika hatua za mwisho na kinachosubiriwa ni vigogo wa pande zote kutoka hadharani kueleza makubaliano yaliyofikiwa.
Taarifa za ndani zilizolifikia Mwananchi zinaeleza baada ya hatua hiyo, utekelezaji unaweza kuanza mara moja huku ACT-Wazalendo kikitarajiwa kutoa mwelekeo mpya kuanzia Mei 3, 2026.
Msingi wa siku 90 za kuundwa kwa SUK unatokana na kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyoitoa Novemba 13, mwaka jana ambapo alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, inataka chama au vyama vya upinzani ambavyo vimepata wajumbe kwenye Baraza la Wawakilishi vipatiwe nafasi katika Baraza la Mawaziri.
Hatua hiyo inaashiria kuwa pande hizo mbili zimekaribia kufikia mwafaka, huku kikao cha kamati kuu cha ACT Wazalendo kitakachofanyika Mei 3 kikipewa uzito mkubwa wa kutoa mwelekeo wa mwisho.
Mmoja wa viongozi wa ACT Wazalendo, kwa masharti ya kutotaja jina lake ameliambia Mwananchi:“Mambo yanakwenda vizuri, subirini mtaona tu mwezi wa tano tunakwenda kuapa niamini kwa hili. Jumapili (Mei 3) tutakuwa na kamati huenda tukajadili suala hili pia,” ameeleza.
Leo Alhamisi Aprili 30, 2026 Mwananchi limezungumza Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita aliyekiri Mei 3 chama hicho, kitakuwa na kamati kuu kitakajadili masuala mbalimbali na huenda SUK likawa mojawapo.
Mchinjita amesema kikao cha kamati ya uongozi kilichoketi jana kikiongozwa na Kiongozi wa chama, Dorothy Semu pamoja na mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud haikujadili suala la SUK bali ajenda zingine zikiwemo za hali ya kisiasa nchini.
Hata hivyo, Mwananchi linafahamu kuwa katika kikao hicho kilichokuwa na wajumbe takribani 12 kiligusia pia suala la SUK ambalo litafikishwa pia katika kikao cha kamati kuu kitakachoketi Jumapili Mei 3.
Kuhusu SUK, Mchinjita amesema kamati maalumu inayosimamia suala hilo ikiongozwa na Othman bado inaendelea na jukumu hilo kama ambavyo ilielekezwa na kamati kuu ya chama hicho.
“Jumapili tutakuwa na kamati kuu nyingine ni maalumu kwa ajili ya masuala mengine, kama kamati ya SUK itakuwa na cha ‘kubrief’ basi itatoa mrejesho,” amesema.
“So far tumefika ambapo kamati ya SUK imesema wamefikia hatua ya makubaliano ya kutambua mambo gani ya msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Mchinjita, hatua iliyofikia kila upande kuyafanyia kazi makubaliano yaliyofikiwa na kwenda kwa umma, kueleza mambo gani yaliyokubaliwa katika mchakato huo, kuliko ilivyokuwa awali.
“Nadhani hatua hiyo ikikamilika kamati zitatoka hadharani nah atua zitakazochukuliwa baada ya hapo.Ikiwa mapema itakuwa bora zaidi, kama kila upande itatekeleza kile tulichokubaliana,” amesema Mchinjita.
Mazungumzo ya kutafufuta muafaka wa kisiasa Zanzibar, yanaongozwa na Othman Masoud Othman na Juma Duni Haji kwa ACT Wazalendo, huku CCM ukiwakilishwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Ali Mohamed Shein.
Machi 14, 2026 Othman ambaye ni mwenyekiti wa ACT Wazalendo aliwaondoa wasiwasi Wazanzibari, akiwataka kuwa watulivu kwa kuwa mazungumzo ya kuleta suluhu ya kisiasa Zanzibar yanaendelea vizuri.
Pamoja na mambo mengi mazungumzo hayo yatakiwezesha ACT Wazalendo SUK, yakifanikiwa kwa mara nyingine chama hicho kitakuwa sehemu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kitakachosubiriwa ni nani atakayetuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, huku wengine watateuliwa kuwa mawaziri kwa nafasi nne zilizoachwa wazi na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Wizara zilizoachwa wazi ni pamoja na Wizara ya Afya, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.