Serikali yazindua mpango mafunzo ya uongoziSerikali yazindua mpango mafunzo ya uongozi

MWANZA :SERIKALI imezindua rasmi Mpango wa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Maafisa Elimu Kata nchini, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa uongozi wa shule, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mei 28, 2026 mkoani Mwanza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa viongozi wa elimu hususan wakuu wa shule za sekondari ambao kwa muda mrefu hawajapata mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa kiwango kinacholingana na mahitaji ya sasa ya mfumo wa elimu.

Amesema tofauti na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wamekuwa wakipata mafunzo ya uongozi, wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakikosa fursa hiyo kwa kipindi kirefu, hali iliyofanya Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha mpango huo wa kitaifa ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa elimu.

“Mpango huu ni fursa muhimu kwa viongozi wa shule kupata maarifa ya kisasa ya uongozi, utawala bora na usimamizi wa elimu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku,” alisema Prof. Nombo.

Prof. Nombo ameeleza kuwa mafunzo hayo hayatawahusu wakuu wa shule pekee, bali yatawajumuisha pia wakuu wasaidizi wa shule za sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha viongozi wote wa elimu wanakuwa na uelewa unaofanana katika kusimamia ubora wa elimu.

Pamoja na hayo ameipongeza ADEM pamoja na VVOB-Tanzania kwa kuandaa na kufadhili mpango huo, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030, jumla ya viongozi wa elimu 16,000 wanatarajiwa kufikiwa, wakiwemo wakuu wa shule na wasaidizi wao 12,000 pamoja na Maafisa Elimu Kata 4,000.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa wakuu wa shule za sekondari, hasa kutokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu kundi hilo halijapata mafunzo ya kina ya kiuongozi na kiutendaji.

Amesema kupitia mafunzo hayo, wakuu wa shule watapata maarifa na mbinu mpya zitakazowawezesha kusimamia shule kwa ufanisi zaidi, kujenga mazingira bora ya kujifunzia na hatimaye kuboresha matokeo ya wanafunzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *