Kenani kuanza ziara Kaskazini, CCM Kilimanjaro yaeleza sababu ya kurejea baada ya miaka 25Kenani kuanza ziara Kaskazini, CCM Kilimanjaro yaeleza sababu ya kurejea baada ya miaka 25

Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimejipanga kuendelea kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kusikiliza kero zao.

Chama hicho kimeeleza kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, baadhi ya majimbo ya mkoa huo yalichukuliwa na vyama vya upinzani, ikiwemo Jimbo la Moshi Mjini.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 28, 2026 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, inayotarajiwa kuanza kesho mkoani humo.

“Kwa historia ya wana Kilimanjaro, sisi tumekuwa waathirika wa upinzani tangu mwaka 1995 baada ya mfumo wa vyama vingi. Baadhi ya majimbo yalichukuliwa na vyama vya upinzani ambavyo havikuwa na hoja,” amesema Boisafi.

Amesema hali hiyo imeanza kubadilika katika miaka ya hivi karibuni kutokana na utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Kwa mfano, Jimbo la Moshi Mjini kwa miaka 25 lilikuwa chini ya upinzani, lakini mwaka 2020 tulilichukua baada ya wananchi kuchoshwa na upinzani na kuona wajaribu upande mwingine,” amesema.

Boisafi amesema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, CCM ilishinda majimbo yote na kata zote isipokuwa Kata ya Kiboriloni, huku katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2025 chama hicho kikishinda maeneo yote yaliyokuwa yakigombewa.

“Wananchi sasa wanajua sehemu ya kupeleka hoja na changamoto zao kwa sababu zinapatiwa ufumbuzi ndani ya chama na serikalini,” amesema.

Akizungumzia ziara ya Kihongosi, amesema inalenga kusikiliza kero za wananchi, kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amesema Kihongosi ataanza ziara yake Wilaya ya Siha kesho, kisha Moshi Mjini na baadaye Wilaya ya Hai Mei 31, akiwa ameambatana na viongozi wa chama pamoja na watumishi kutoka ofisi za Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yatakayojitokeza.

“Kesho ataanza Wilaya ya Siha ambapo atatembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro, Hospitali ya Kibong’oto, shina namba tisa kuangalia uhai wa chama na kufanya mkutano wa hadhara eneo la Sanya Juu karibu na kituo cha mabasi,” amesema.

Aidha, amesema CCM itaendelea kueleza wananchi utekelezaji wa ahadi zake badala ya kujikita katika malumbano ya kisiasa.

“Tunawaomba wananchi wa mkoa huu, bila kujali chama au dini zao, wajitokeze kusikiliza mambo yaliyofanywa. Huko nyuma tulikuwa waathirika hapa Moshi Mjini, lakini sasa mambo yamebadilika,” amesema.

Baada ya kumaliza ziara mkoani Kilimanjaro, Kihongosi ataendelea na ziara katika wilaya za Hanang, Babati na Simanjiro mkoani Manyara kabla ya kuhitimisha katika wilaya za Karatu, Arumeru na Arusha Mjini.

Awali, Kihongosi alianza ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *