
Dodoma. Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema hakuna kilimo chenye tija bila uwepo wa mbegu bora pamoja na mifumo imara ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu kwa wakulima.
Silinde amesema hayo leo Alhamisi Mei 28, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa tasnia ya mbegu nchini uliojadili namna ya kuimarisha mifumo ya mbegu kwa usalama wa chakula na biashara.
Amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kibiashara, shindani na yenye kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa Watanzania.
Amesema Wizara ya Kilimo imeendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali ikiwemo kuongeza bajeti ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za ndani ili kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesema matumizi ya mbegu bora nchini yameongezeka kutokana na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kupitia taasisi kama Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) pamoja na kampuni binafsi za mbegu.
“Hakuna kilimo chenye tija bila mbegu bora na mifumo thabiti ya uzalishaji na usambazaji,” amesema Silinde.
Katika hatua nyingine, Silinde amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ruzuku za pembejeo yameongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa mbegu na mbolea kwa wakulima.
Pia, amepongeza ushiriki wa Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika uzalishaji wa mbegu kwa wingi kupitia mashamba yao, hatua aliyosema imechangia kuimarisha upatikanaji wa mbegu nchini.
Kutokana na hali hiyo, Silinde amezitaka kampuni za mbegu kujikita katika uzalishaji wa mbegu zinazostahimili ukame na magonjwa ya mazao huku taasisi za kifedha zikihimizwa kuweka mikopo yenye riba nafuu kwa wazalishaji wa mbegu na wakulima.
Aidha, ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi kuendelea kusisitiza mikoa na wilaya kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu.
“Tunaipongeza Wilaya ya Tanganyika kwa kutenga hekta 17,000 kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu,” amesema Silinde.
Mkurugenzi wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kuisimamia na kuiwezesha sekta ya mbegu nchini.
Amesema kupitia maelekezo na miongozo mbalimbali ya serikali, wadau wa sekta ya mbegu wameendelea kupata dira sahihi ya utekelezaji wa majukumu yao.
“Tunathamini sana mchango wa Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha tasnia ya mbegu inaendelea kuimarika na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo,” amesema Chimagu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Justina Rahi amesema matumizi ya pembejeo bora ni suluhisho muhimu la kuongeza uzalishaji kwa wakulima.
Amesema bado gharama za uzalishaji ni kubwa kwa wakulima wengi, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu.
“Tunawaomba wadau na watafiti kuendelea kuzalisha mbegu zinazostahimili ukame, magonjwa pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Rahi.
