​Wakati dunia ikiendelea kupiga hatua katika usawa wa kijinsia, utafiti mpya uliofanywa katika nchi 16 barani Afrika umeibua ukweli mchungu kuhusu uwezo wa mwanamke aliyeolewa kumiliki mwili wake na uamuzi kuhusu uzazi.

Ripoti hiyo ya afya ya jamii inaashiria kuwa, licha ya jitihada za kimaendeleo, mamilioni ya wanawake kusini mwa jangwa la Sahara bado wapo chini ya shinikizo la mfumo dume, mila na shinikizo la ndugu katika kufanya uamuzi wa msingi kuhusu afya yao ya uzazi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaripoti kuwa wanawake milioni 164 kote ulimwenguni wana uhitaji wa uzazi wa mpango ambao haujafikiwa, na mwanamke mmoja kati ya watatu amewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au wa kijinsia katika maisha yake.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wanawake milioni 257 duniani kote hulazimishwa na wenza wao kushiriki ngono bila uwezo wa kujadiliana kuhusu matumizi ya kondomu au kufanya uamuzi juu ya huduma zao za afya ya uzazi.

Hali ilivyo sasa

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 37 tu ya wanawake katika kanda hii wenye uwezo wa kufanya uamuzi sahihi kuhusu uhusiano wa kijinsia, matumizi ya kinga, na huduma za afya. 

Hali hii ni tofauti kabisa na mataifa ya Ulaya ambako asilimia 87 ya wanawake wana uhuru kamili wa kujiamulia masuala hayo.

​Wataalamu wanabainisha kuwa kukosekana kwa uhuru huu kunachangia mwanamke kushindwa kuendelea na masomo, kukwama kiuchumi, na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na ujauzito usiotarajiwa au upataji mimba usio salama.

​Utafiti huo uliowahusisha wanawake zaidi ya 67,000, umebaini kuwa elimu ndiyo silaha kuu. Wanawake waliopata fursa ya kufika elimu ya sekondari na kuendelea, walionekana kuwa na sauti na uthubutu wa kujadiliana na wenza wao kuhusu uzazi wa mpango kuliko wale wasio na elimu.

Vilevile, uhuru wa kifedha umetajwa kuwa nguzo muhimu. Mwanamke mwenye ajira ya kulipwa na anayemiliki akaunti ya benki ana uwezekano mkubwa wa kusikilizwa na kuheshimiwa katika uamuzi ya familia, tofauti na yule anayemtegemea mwenza wake kwa kila kitu.

Mapinduzi ya kidijitali

Jambo la kuvutia katika ripoti hiyo ni mchango wa teknolojia. Upatikanaji wa huduma za mtandao na matumizi ya simu za mkononi kwa miamala ya fedha imetajwa kumpa mwanamke ulimwengu mpya wa habari. 

Kupitia simu, wanawake sasa wanapata elimu ya afya ya uzazi kwa usiri na urahisi, jambo linalowasaidia kufanya uamuzi bila hofu ya kuhukumiwa na jamii.

Katika nchi zilizofanyiwa utafiti, Madagascar na Uganda zimetajwa kuongoza kwa kuwa na wanawake walioolewa wenye uthubutu mkubwa wa kusema “ndiyo” au “hapana” katika masuala ya uzazi.

 Katika upande wa pili, nchi kama Benin zimebaki nyuma, huku mfumo wa kijamii ukiendelea kuminya haki hizo.

Watafiti wanashauri kuwa ili kuboresha afya ya mwanamke, serikali hazina budi kuwekeza nguvu nyingi katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha huduma za kidijitali zinafika hadi vijijini. 

Hii itasaidia kuvunja minyororo ya utegemezi ambayo kwa muda mrefu imekuwa kikwazo cha mwanamke kumiliki afya yake mwenyewe.

Makala hii awali ilichapishwa kwa Kiingereza katika mtandao wa The Conversation.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *