IMEFICHUKA kuwa nyota wa Simba, Anicet Oura hakupata majeraha makubwa kama ilivyodhaniwa katika fainali ya Kombe la Muungano, bali benchi la ufundi la timu hiyo lilifanya uamuzi wa kimkakati kumpumzisha kwa ajili ya ‘kazi maalumu’ katika dabi ya keshokutwa Jumapili dhidi ya Yanga.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Oura alionekana kushika paja na kushindwa kuendelea, hali iliyozua hofu kwa mashabiki wa Simba kabla ya kocha Steve Barker kufanya mabadiliko na kumpa nafasi Seleman Mwalimu ambaye aliibuka shujaa kwa kufunga bao la ushindi katika dakika ya 119 na kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo.
Akizungumza kuelekea mchezo huo mkubwa wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Barker aliweka wazi kuwa hawakuwa tayari kuhatarisha nyota huyo muhimu.
“Hatukutaka kuhatarisha afya yake, Oura alikuwa na maumivu madogo, lakini tuliona ni busara kumpumzisha ili awe tayari kwa mchezo wa Jumapili ambao nao ni muhimu kwetu,” amesema Barker.
Aliongeza kuwa: “Hii ni dabi, mechi ambayo inahitaji wachezaji kuwa kwenye kiwango cha juu kabisa. Tunamhitaji Oura pamoja na wachezaji wengine wakiwa fiti kwa asilimia mia moja.”
Oura ambaye tayari ana mabao matatu katika Ligi Kuu Bara, ameonyesha kuwa moja ya silaha muhimu ndani ya kikosi cha Simba tangu alipojiunga na timu hiyo Januari 2026 akitokea IF Gnistan ya Finland.
Uwezo wake wa kushambulia na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wengine umemfanya kuwa mchezaji muhimu kwa wekundu hao wa Msimbazi. Simba inaingia kwenye dabi hiyo ikiwa na presha ya ushindi ili kupunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao Yanga kutoka tano hadi mbili. Kwa sasa, Yanga wanaongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 47 huku Simba ikifuatia na pointi 42, zote zikiwa zimecheza mechi 19.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa Zanzibar, timu hizo zilitoka suluhu, kabla ya kukutana tena katika fainali ya Kombe la Muungano ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Mwalimu.
VITI VYAONGEZWA ISAMUHYO
Wakati presha ya dabi ikizidi kupanda, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaendelea na maboresho ya haraka ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuhakikisha unakuwa tayari kwa mchezo huo.
Katika maboresho hayo, viti vipya 2,000 vinaongezwa ili kuongeza uwezo wa uwanja kutoka mashabiki 10,000 hadi 12,000, hatua inayolenga kukidhi wingi wa mashabiki wanaotarajiwa kufurika kushuhudia dabi hiyo ya watani wa jadi. Meneja wa uwanja huo, Said Mpuche, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na kila kitu kitakuwa tayari kabla ya filimbi ya kuanza kupulizwa.
Dabi hiyo ya Jumapili inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya uwanja huku viingilio vikiwa Sh15,000 kwa kawaida (mzunguko), VIP B Sh30,000 na VIP A Sh50,000.