Taarifa ya MONUSCO iliyochapishwa kwenye wavuti wake inasema kuwa walinda amani wa MONUSCO kutoka vituo vya operesheni vya Fataki na Gina waliokoa watu hao ambao walinasa katikati ya mapigano hayo siku ya Jumanne baada ya waasi hao kushambulia makao makuu ya kikosi cha Jeshi la serikali FARDC huko Pimbo.

Kilichotokea na hatua zilizochukuliwa

Shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa wa mali katika kambi ya kijeshi.

MONUSCO inasema mapigano pia yalizuka kati ya wafuasi wa CRP na wanamgambo wa CODECO katika eneo hilo hilo.

“Wakiwa wamejikuta katikati ya mapigano, takribani watu 200 walilazimika kukimbia makazi yao kwa haraka, na kujikuta wakikabiliwa moja kwa moja na risasi. Wengi wao walikuwa wanawake na watoto,” imesema taarifa hiyo.

Baada ya kuarifiwa, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka vituo vya Fataki na Gina walifika haraka katika eneo la tukio.

“Walipowasili, waliratibu hatua zao na FARDC pamoja na mamlaka za eneo hilo ili kudhibiti vurugu, kulinda eneo, na kuwasaidia raia.”

Huduma baada ya kuokolewa

Raia hao walipewa hifadhi kwanza katika jengo la shule huko Pimbo kabla ya kusindikizwa kwa usalama hadi katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Gina.

Wakiwa huko, walihudumiwa na kukabidhiwa kwa mamlaka za eneo hilo, ikiwa ni pamoja na chifu wa kundi na kiongozi wa wakimbizi, sambamba na kupatiwa ulinzi wa kutosha.

Mmoja wa wakimbizi hao, Claude Mateso amenukuliwa akisema “leo, hali imerejea kuwa tulivu, mbali na vurugu za jana. Watu waliokimbia makazi yao waliokuwa katika eneo hili wamehamishwa hadi Gina na MONUSCO katika hali ya usalama. Tunapongeza hatua yao ya haraka pamoja na ushirikiano wao na FARDC. MONUSCO inaendelea kuwa karibu na wananchi na iko tayari kila inapopewa taarifa.”

Kwa sasa MONUSCO inaendelea na doria za usiku na mchana huko Pimbo na maeneo ya jirani ili kuhakikisha usalama kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *