
KOCHA wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema matokeo ya Zanzibar hayahusiani na mechi ya kesho dhidi ya Simba kwani ni mashindano ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Aprili 29, 2026, Yanga ilipoteza ubingwa wa Kombe la Muungano baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kesho Jumapili, ni takribani siku nne zimepita tangu watani hao wa jadi watoke kucheza fainali hiyo ambapo sasa wanakutana katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Pedro amesema baada ya kupoteza mechi iliyopita, wamerejea wakiwa imara na wanafahamu umuhimu wa kushinda kesho dhidi ya Simba.
“Ni mashindano tofauti, tunajiamini vya kutosha na tunaamini tunaweza kucheza vizuri kesho, tunaenda kucheza mechi na moja ya timu ngumu Tanzania na Afrika,” amesema Pedro.
Kwenye mechi hiyo, Yanga itamkosa kiungo Mudathir Yahya kutokana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu baada ya kumchezea faulo mchezaji wa Pamba Jiji.
Pedro amesema: “Sijafurahia hiyo hali lakini sio mara ya kwanza kucheza bila ya Mudathir, hivyo tumefokasi na mechi ya kesho.”
Beki wa kushoto wa Yanga, Mohamed Hussein, amesema: “Kesho tunaenda kucheza mchezo mkubwa na tunatambua ubora wa wapinzani wetu, hivyo kila mchezaji amejipanga kuhakikisha anafanya vizuri.
“Tukipoteza mchezo wa kesho itakuwa tumetofautiana pointi mbili na wapinzani wetu na tunajua tukishinda kesho inaamaana tutakuwa tumezidi kusogea kwa hiyo ni mechi ngumu sana.”
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 47, inafuatia Simba yenye 42, hivyo matokeo ya ushindi kwa yeyote, itaiweka timu nafasi nzuri zaidi.