ILIPOISHIA

Kwa sekunde kadhaa alikuwa ameduwaa akimtazama Masumbuko bila kupepesa. Sharifa aliyekuwa ameketi kando yake hakuwa akijua hisia zilizokuwema ndani ya akili ya mwanawe. Hakuwa akimjua Masumbuko na hakuwahi kumuona. Hivyo alishanagaa alipomuona Majaliwa ameduwaa.

“Unaweza kumtambua mtu aliyekupiga risasi kule gesti siku ile?” Wakwetu alimuuliza Masumbuko.

SASA ENDELEA…

“Ni kama huyu aliyeko hapa,” Masumbuko alisema huku akimwonesha Majaliwa.

Uso wa Wakwetu ulihamaki, akaenda kumshika mkono Majaliwa na kumuinua kwenye kochi.

“Twende!” alimwambia na kutoka naye nje.

Walipofika nje ya nyumba, alimuuliza:

“Niambie ukweli, ni kwa nini siku ile uliiba gari yangu na bastola yangu na kwenda kumpiga risasi yule kijana?”

Majaliwa aliinamisha uso wake chini na kunyamaza kimya.

“Tafadhali niambie. Ile kesi bado ipo. Nataka jibu lako. Kama hutaniambia, nakupeleka polisi.”

“Nitakwambia,” Majaliwa alisema akiwa ameinamisha uso wake chini.

“Niambie.”

Majaliwa akaueleza ukweli wote, mwanzo hadi mwisho. Wakwetu akajua kwamba Majaliwa alikuwa mtoto wa mke wake na kwamba alikuwa amembambikia. Pia alijua kuwa njama za kumuua Masumbuko alizipanga yeye na mama yake ili yeye, Wakwetu, asimgundue mtoto wake halisi.

Wakwetu alipopata ukweli huo alirudi ndani, sasa akiwa amepandisha mori.

“Sasa nimeshapata ukweli uliokuwa ukisumbua akili yangu kwa muda mrefu kuhusu wewe na huyu mtoto,” Wakwetu alimwambia mke wake kwa hasira.

Sharifa, kwa kujua bomu lilikuwa limeshapasuka, alinyamaza kimya.

“Nimeshajua kwamba huyu Majaliwa ni mwanao mwenyewe. Mlikula njama ukamleta hapa ili anidanganye kuwa ni mwanangu wakati si kweli. Leo nimekwenda kufanya vipimo hospitalini, ikabainika kuwa si mwanangu,” Wakwetu aliendelea kumpasha Sharifa.

Akaendelea:

“Baya zaidi, mbali na kufuja mali zangu na kunifanyia kila aina ya ufisadi, mlipanga njama Majaliwa amuue mwanangu ili mpango wenu usifichuke. Lakini Mungu ni mkubwa, mpango wenu umeshindikana na njama zenu zimebainika. Mwanangu wa halali amejulikana leo, na si mmoja, ni wawili.”

Wakwetu akamtazama James.

“Nilimuajiri James bila kujua kuwa ni mwanangu. Leo nimewabaini wanangu. Namshukuru Mungu,” akasema.

Sharifa aliinua uso akamtazama James. James akainamisha uso wake chini.

“Mwanao alimnyanyasa sana mwanangu wakati akiwa dereva, alifikia hata kumpiga makofi akijifanya yeye ndiye mwenye haki hapa. Kwa kweli nimepata huzuni sana!” Wakwetu aliendelea kumweleza Sharifa.

“Kama ulikuwa na mtoto na ulipenda tumlee, ungeniambia tu kuliko kutumia njia za ghiliba, uongo na ukatili wa kutaka kumuua mwanangu. Nimegundua wewe mwanamke si mwema wangu. Usingethubutu kufikiria kumuua mwanangu. Naona hata mimi pia unaweza kuniua!” Wakwetu sasa alisema kwa kufoka.

“Uliiba bastola yangu ukampa mtoto wako pamoja na gari, halafu ukajifanya hujui kitu.”

Alipofika hapo Wakwetu alitoa kicheko cha uchungu na huzuni. Wakati anacheka sauti yake ilikuwa ikiunguruma kama aliyekuwa amebanwa mbavu. Ilikuwa hasira iliyokuwa ikiwaka kwenye moyo wake.

Wakwetu alipoacha kucheka aliwatazama James na Masumbuko.

“Wanangu, karibuni nyumbani kwenu. Hapa ndiyo kwenu. Mmehangaika kwa miaka mingi kama meli iliyokuwa ikisukumwa na dhoruba na kukosa bandari ya kutua, hatimaye leo dhoruba imekoma na mmeipata bandari,” Wakwetu aliwaambia wanawe kwa furaha.

“Wewe uliyekuwa dereva wangu, sasa hivi si dereva wangu tena, na wewe uliyekuwa yatima, sasa hivi si yatima tena. Mmeshampata baba yenu, ni mimi hapa, Wakwetu, na hapa ndiyo kwenu. Mimi nikifa, nyinyi ndiyo mtarithi mali yangu, si mwingine,” aliendelea kuwaambia.

“Asante, baba,” wote wawili wakasema kwa pamoja.

Wakwetu akamgeukia Sharifa.

“Sasa Sharifa, umeshapoteza sifa ya kuwa mke wangu na Majaliwa ameshapoteza sifa ya kuwa mwanangu. Kutoka leo mnaondoka hapa nyumbani.

“Chukueni kila kilichokuwa chenu muondoke, wewe si mke wangu tena!”

Sharifa alipiga magoti mbele ya Wakwetu.

“Mume wangu, naomba unisamehe…” akasema kwa kigugumizi cha huzuni.

“Eti nini… mimi nikusamehe wewe! Umefanya kosa lisilosameheka. Tayari ulikuwa umeshanipachika mtoto asiye wangu na tayari mlikuwa mmepanga njama za kumuua mwanangu asiye na kosa… sitakusamehe!” Wakwetu alimwambia kwa sauti kali.

“Mume wangu, naomba unisamehe, ni ibilisi tu aliyekuwa ametupitia,” Sharifa aliendelea kumbembeleza.

“Kama mwanangu angekufa pia ingekuwa ni ibilisi amempitia? Usinieleze upuuzi huo. Mimi nimeshakuacha, wewe si mke wangu tena. Tena nimekuacha talaka tatu kwa mpigo kwa maana sina nia ya kukurudia tena.”

Sharifa akajishika kichwa.

“Mume wangu, umenimaliza…!”

“Sasa twende ukafungashe virago vyako.”

Wakwetu alimshika mkono Sharifa akamuinua na kuingia naye chumbani.

“Chukua vitu vyako uondoke humu ndani.”

“Mume wangu, nitakwenda wapi usiku huu?”

“Mimi si mume wako tena, tafadhali niite jina langu. Naitwa Wakwetu. Kujua mtakwenda wapi si juu yangu.”

Sharifa alipoona Wakwetu amechachamaa akaanza kufungasha. Kazi hiyo aliifanya kwa taratibu sana. Ikamchukua karibu saa nzima. Wakati wote Wakwetu alikuwa amemsimama kando yake akimsubiri.

Sharifa alipoteza muda ili kumpa nafasi Wakwetu ya kuufikiria uamuzi wake wa kumuacha. Alidhani huenda Wakwetu angeweza kubadili mawazo na kumsamehe.

Lakini hadi anajaza masanduku yake mawili, Wakwetu hakumtamkia kitu chochote. Walitoka sebuleni, Wakwetu akamfungulia mlango wa mbele.

“Safari njema,” akamwambia.

Sharifa akamtazama James.

“Kwaheri, James,” alimuaga, halafu akajisemea peke yake, “Sijui nitakwenda wapi usiku huu na nitaibeba na nini mizigo hii.”

“Baba, naomba unisikilize,” James akamwambia baba yake.

Wakwetu alimsogelea na kumuuliza:

“Unasemaje?”

“Ni kweli kwamba tatizo limetokea, lakini mlipooana na mama mlioana kwa wema na ni vizuri wakati huu mnapoachana muachane kwa wema. Mama amekuhudumia kwa muda wote, kwa nini leo usimpe kitu cha kwenda kuanzia maisha mengine au kwa nini mama leo asipate japo usafiri wa kumpeleka anakokwenda?” James akamwambia baba yake.

Maneno yake yakamuingia Wakwetu, akataka pia kusikiliza maoni ya Masumbuko.

“Unasemaje, Masumbuko?”

“Licha ya kwamba mimi ndiye ambaye ningekufa kama ile risasi ingenipata mahali pabaya, lakini bado Mungu anatwambia tusilipe baya kwa baya. Mtendee wema hata mtu ambaye alikufanyia ubaya na ikiwezekana msamehe. Lakini kwa vile umeshamuacha mama, talaka tatu haziwezi kurudi, mimi pia ninakuomba umuache mama kwa wema kwa sababu alikuwa mke wako.”

“Nimewasikiliza wanangu na ombi lenu nitalitekeleza,” Wakwetu aliwaambia.

Aliingia chumbani. Baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika kitita cha noti nyekundu.

“Mimi nampa laki tatu, zitamsaidia kwa usafiri wa huko anakokwenda na pia kuanzia maisha,” akasema na kumpa pesa hizo Sharifa.

Sharifa alizipokea na kushukuru, akatoka nje huku akisindikizwa na Wakwetu. Walikutana na Majaliwa mbele ya mlango. Majaliwa alimpokea mama yake sanduku moja. Wakafunguliwa geti na mlinzi.

Wakiwa nje ya geti, Sharifa alitoa simu yake akampigia dereva wa teksi aliyekuwa akimfahamu. Baada ya nusu saa teksi ikafika.

“Tunakwenda wapi?” Majaliwa akamuuliza mama yake wakati wanajipakia kwenye teksi.

“Itabidi twende Chumbageni kwa mjomba wako.”

“Kutakuwa na nafasi ya kukaa sisi?”

“Tutakwenda kujua huko huko.”

Walifunga milango. Teksi ikaondoka.

Wakiwa kwenye teksi ndipo Sharifa alipoanza kuyafikiria maisha mapya anayokwenda kuyaanza. Akamtazama mwanawe Majaliwa na kuanza kujuta kimoyomoyo kuhusu vitendo vyake vya tamaa ambavyo hatimaye vimemharibia maisha.

Teksi ikafika kwa kaka yake Chumbageni, wakashuka. Walipoingia ndani kaka yake akashituka kuona wageni wakiwa na mizigo. Sharifa akamweleza yaliyotokea.

“Ni mgeni wa siku mbili tu. Sitakaa sana hapa,” akamsisitizia kaka yake baada ya kumweleza mkasa uliomkuta.

“Unatarajia kwenda wapi?”

“Nitarudi Kwaaminchi nikaendelee na biashara yangu ya chipsi.”

Wiki haikumalizika akahamia Kwaaminchi pamoja na mwanawe. Wakaanzisha tena mradi wa chipsi.

Haukupita hata mwezi mmoja Sharifa akakutana na Mashaka Msumari aliyemtongoza, wakakubaliana na kupanga kuoana. Baada ya uchumba wa mwezi mmoja wakaoana na Sharifa akahamia Usagara ambako Mashaka alikuwa anakaa.

Maisha hayakuwa mabaya. Mashaka alikuwa meneja wa kampuni binafsi. Alikuwa akiishi katika nyumba ya kampuni.

Mtu wa kwanza kufahamiana naye katika mtaa uliokuwa na nyumba yetu ni Mwanaisha, mke wa jamaa mmoja aliyekuwa jirani yetu. Mwanaisha akaja kuwa rafiki yangu mkubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *