Marekani kwa sasa ina zaidi ya wanajeshi 36,000 nchini Ujerumani

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amesema kuwa uamuzi wa Marekani kuondoa wanajeshi 5,000 kutoka nchini humo ulikuwa “unatarajiwa”, huku muungano wa kijeshi wa NATO ukisema unatafuta ufafanuzi zaidi kutoka Washington.

Akizungumza na shirika la habari la DPA, Pistorius alisisitiza kuwa “uwepo wa wanajeshi wa Marekani barani Ulaya, na hasa nchini Ujerumani, ni kwa manufaa yetu na pia ni kwa manufaa ya Marekani”.

Wakati huo huo, msemaji wa NATO, Allison Hart, alisema kuwa muungano huo “unafanya kazi na Marekani kupata maelezo ya uamuzi huo”.

Alipoulizwa kuhusu kuondolewa kwa wanajeshi hao, Rais wa Marekani Donald Trump alisema: “Tutapunguza kwa kiwango kikubwa, na tutapunguza zaidi ya hao 5,000.” Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.

Hatua hiyo ya Washington imekuja baada ya Trump kumkosoa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kwa kauli yake kwamba Marekani “imedhalilishwa” na wajumbe wa Iran katika vita vinavyoendelea.

Kwa sasa, uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Ujerumani unazidi wanajeshi 36,000 walioko kazini, ukiwa ndio mkubwa zaidi barani Ulaya, ukilinganishwa na takribani wanajeshi 12,000 walioko Italia na 10,000 walioko Uingereza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *