.

Chanzo cha picha, VCG via Getty Images

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa miongo kadhaa iliyopita, China imeendelea kuficha na kutoweka wazi kuhusu ukubwa wa hifadhi yake ya silaha za nyuklia na sera zake zinazohusiana nazo.

Msimamo rasmi wa China ni kwamba sera yake ya nyuklia inalenga hasa ulinzi wa taifa. Kwa muda mrefu imekuwa ikisisitiza sera ya “kutotumia silaha za nyuklia kwanza ikimaanisha kuwa China haitaanza kutumia silaha za nyuklia katika vita, bali itazitumia tu kujibu shambulio la nyuklia dhidi yake.

Hata hivyo, China imekuwa ikikataa wito wa kushiriki katika mazungumzo ya pande tatu kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia pamoja na Marekani na Urusi.

Wachambuzi wa kutoka mataifa ya magharibi wameelezea kuwa China imekuwa ikiboresha uwezo wake wa silaha za nyuklia katika miaka ya hivi karibuni. Makadirio yanaonyesha kuwa kati ya mwaka 2023 na 2025, China imekuwa ikiongeza takriban silaha 100 za nyuklia kwenye hifadhi yake kila mwaka.

China imeboresha mfumo wake wa makombora na miundombinu inayohusiana nayo ili kuongeza uwezo wake wa kujibu mashambulizi yoyote yanayoweza kutokea.

Beijing inasema kuwa uwezo wake wa silaha za nyuklia upo kwa madhumuni ya kuzuia maadui kufanya mashambulizi, na kwamba haitasita kuonyesha uwezo wake wa nyuklia iwapo kutatokea shambulio lolote la nyuklia dhidi yake.

Mwaka 2024, China ilifanya jaribio la kombora la masafa marefu linaloweza kuvuka mabara tofauti katika bahari ya Pasifiki. Kisha mwaka 2025, kwa mara ya kwanza ilionyesha hadharani mfumo wake wa nyuklia wa nguzo tatu katika gwaride la kuadhimisha kumbukumbu ya vita vya pili vya dunia.

Mfumo huo unajumuisha silaha za nyuklia zinazoweza kurushwa kutoka nchi kavu, baharini na angani, hivyo kuongeza uwezo wa China wa kujibu shambulio lolote la nyuklia.

Sera ya China

.

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Msimamo rasmi wa China umekuwa kwamba sera yake ya nyuklia ni ya kujilinda.

Mwaka wa 2024, China iliwasilisha mpango uitwao “Mpango wa Kutotumia Silaha za Nyuklia Kwanza, ambao ilisema ni “hatua ya kivitendo” ya kutekeleza Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

China pia ilitoa wito kwa mataifa yenye silaha za nyuklia kupitisha sera ya kutotumia silaha hizo kwanza na kuahidi kutotumia wala kutishia kutumia silaha za nyuklia dhidi ya mataifa yasiyo nazo.

Tathmini ya mataifa ya Magharibi

Licha ya sera ya China kuwa na utata kuhusu silaha za nyuklia, wachunguzi kutoka mataifa ya Magharibi wamebaini katika miaka ya hivi karibuni kuwa China inaboresha kwa kasi uwezo wake wa silaha za nyuklia.

Ripoti ya hivi karibuni ya kila mwaka ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI), inakadiria kwamba hifadhi ya silaha za nyuklia ya China iliongezeka na kufikia takriban silaha 620 za nyuklia kufikia Januari mwaka wa 2026, ikilinganishwa na silaha 600 mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa SIPRI, China iliongeza silaha 90 za nyuklia kwenye hifadhi yake kati ya mwaka 2023 na 2024, na silaha 100 kati ya 2024 na 2025. Ongezeko hili lilikuwa la kasi zaidi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, ingawa kasi hiyo imeanza kupungua.

Ripoti ya Pentagon ya mwaka 2024 ilikadiria kuwa China inaweza kuongeza mara mbili hifadhi yake ya silaha za nyuklia na kufikia zaidi ya silaha 1,000 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, makadirio haya hayakujumuisha utabiri wa awali wa ripoti ya mwaka 2022, uliodai kuwa hifadhi ya China inaweza kufikia takriban silaha 1,500 ifikapo mwaka 2035

Maonyesho ya uwezo wa nyuklia

.

Chanzo cha picha, VCG via Getty Images

Ingawa vyombo rasmi vya habari vya serikali ya China huepuka kutoa maoni kuhusu takwimu za mataifa ya Magharibi, Beijing imekuwa ikionyesha wazi uwezo wake wa nyuklia katika miaka ya hivi karibuni, kama ilivyotokea mwaka 2024 ilipofanya majaribio ya kombora la masafa marefu linaloweza kuvuka mabara katika bahari ya pasifiki kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka 44.

Wizara ya Ulinzi ya China haijatoa taarifa rasmi kuhusu majaribio hayo, lakini vyombo vya habari vya China viliripoti kuwa kombora hilo liligonga lengo lililokuwa umbali wa kilomita 2,000, huku likiwa na uwezo wa kusafiri hadi kilomita 12,000.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, kombora hilo linaweza kufika eneo la South Pole, bara lote la Ulaya, na miji yote mikubwa ya Pwani ya Magharibi ya Marekani.

Kulingana na mtaalamu wa ulinzi wa China, Du Wenlong, jaribio hilo linaonyesha uwezo wa China wa kushinda mifumo yoyote ya ulinzi wa anga na ya kukinga makombora.

Katika gwaride la kijeshi la kuadhimisha miaka 80 ya ushindi dhidi ya Japani mwaka 2025, Beijing ilionyesha kwa mara ya kwanza mfumo wake wa nyuklia wa pande tatu, ardhini, angani na baharini.

Vyombo vya habari vya China vilieleza mfumo huo kama “nguvu ya kimkakati.” Mfumo huo ulijumuisha kombora la masafa marefu linalorushwa kutoka angani, kombora la nyuklia la masafa marefu linalorushwa kutoka manowari, kombora la kurushwa kutoka ardhini, pamoja na kombora la nyuklia la masafa marefu linalotumia mafuta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *