
Moshi/Nairobi. Raia wa Tanzania, Anthony Juma maarufu Kipara, anashikiliwa na vyombo vya dola nchini Kenya, akituhumiwa kuhusika na mauaji ya kikatili ya mtoto Glorious Maore mwenye umri wa miaka 11 nchini humo.
Kipara anakuwa Mtanzania wa pili ndani ya mwezi mmoja, baada ya msanii wa Tanzania, Sefu Shabani maarufu Matonya (43), kukamatwa nchini humo kwa tuhuma za kumbaka mwanamke raia wa Kenya.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) nchini Kenya, Aprili 29, mahakama ilimwachia kwa dhamana mwanamuziki huyo baada ya kuweka bondi ya KSh 500,000, sawa na Sh10 milioni za Tanzania, na kukabidhi pasi ya kusafiria.
Tukio analotuhumiwa nalo lilitokea Aprili 7, 2026 katika makazi yaliyopo Nyali, Kaunti ya Mombasa, na alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkuu, Robinson Ondiek wa Mahakama ya Sanzu, Jiji la Mombasa, na kukanusha mashtaka hayo.
Wakati tukio la Matonya likiwa bado linagonga vichwa vya mashabiki wake ndani na nje ya nchi kuhusu tukio hilo lililomfanya asote mahabusu kwa siku 19, Mtanzania mwingine anashikiliwa nchini humo kwa tuhuma za mauaji.
Kesi dhidi ya Mtanzania huyo imepangwa kutajwa kesho, Mei 4, 2026, na hii ni baada ya Aprili 13, 2026, mahakama kutoa agizo la kuzuiliwa kwake mahabusu kwa siku 21 ili kuwezesha wapelelezi kukamilisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Taarifa ya DCI Kenya
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya, aliyoitoa Mei mosi, 2026 kupitia ukurasa rasmi wa X (zamani Twitter), mtoto aliyeuawa alinajisiwa kwanza kabla ya kunyongwa hadi umauti ulipomfika.
DCI alidai katika taarifa hiyo kuwa kilichoanza kama msako mkali wa kumtafuta mtoto aliyetoweka kilihitimishwa kwa kukamatwa kwa Kipara, anayedaiwa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Glorious.
DCI anadai mtoto huyo aliripotiwa kutoweka Machi 15, 2026, baada ya kutorejea nyumbani kutoka kwenye mazoezi ya shule ya Jumapili (Sunday School), hali iliyoibua simulizi.
Watoto wanagundua mwili wa Glorious
Taarifa ya DCI inadai kuwa siku kadhaa baada ya mtoto huyo kutoweka, mwili wake uligunduliwa na watoto katika eneo la Manyani ukiwa umetelekezwa.
“Siku kadhaa baadaye, katika eneo la Manyani, ugunduzi wa kutisha ulipatikana wakati watoto waliokuwa wakicheza karibu na hapo walipojikwaa na gunia lililokuwa na mkono wa binadamu ukichomoza kutoka humo,” imedai taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya DCI Kenya, maofisa wa polisi walijulishwa, na baada ya ukaguzi, mwili usio na uhai wa msichana mdogo ulipatikana ndani, umefungwa kwa kamba katika jaribio la makusudi la kuficha uhalifu.
“Uchunguzi wa postmortem uliofanywa katika Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani ulithibitisha kuwa Glorious alikuwa amenajisiwa kabla ya kunyongwa hadi kufa, ukiukaji wa kutisha wa kutokuwa na hatia,” ameongeza kudai DCI.
“Maofisa wa upelelezi kutoka Kisauni walianzisha uchunguzi mara moja, wakiunganisha nyuzi muhimu ambazo zilielekeza kwa Anthony Juma, maarufu Kipara, kama mshukiwa mkuu,” amedai katika taarifa hiyo na kuongeza kuwa:
“Hata hivyo, mshukiwa huyo alikuwa amekimbia, akiacha nyumba iliyotelekezwa na nguo na vitanda vilivyokuwa vimeungua sehemu vilipatikana, ikiashiria uwepo wa jaribio lililofeli la kuharibu vielelezo muhimu vya tukio hili,” amesema.
DCI ameeleza kuwa msako ulianza Aprili 12, 2026, na mshukiwa alikamatwa, na baadaye kufikishwa mahakamani, ambapo wapelelezi waliomba amri ya kumshikilia kwa siku 21 ili kuruhusu upelelezi kukamilika.
Aprili 13, 2026, mahakama ilikubali ombi hilo na kutoa agizo la kuzuiliwa kwake kwa siku 21, kuwezesha wapelelezi kukamilisha uchunguzi.
Mtuhumiwa huyo, ambaye ni raia wa Tanzania anayedaIwa kufanya kazi ya kuzoa taka bila kuwa na kitambulisho rasmi, anaendelea kuzuiliwa huku upelelezi ukiendelea. Kesi hiyo itatajwa kesho, Jumatatu Mei 4, 2026, ili kupata mwenendo wa upelelezi.