Arusha. “Wako wapi?” Ndilo swali linaloendelea kuumiza vichwa vya ndugu na jamaa wa Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka (22), maarufu kama ‘Rahma’ wanaodaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Juni 20, 2025 mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa za familia, wasichana hao waliondoka nyumbani wakiaga kwenda kwenye sherehe ya Kareen ya kuhitimu mitihani ya mwaka wa kwanza, lakini hawakurudi tena na hawajawahi kuonekana hadi sasa.

Hata hivyo, tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tengeru na kupewa jalada namba TEG/RB/342/2025.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi jana Jumamosi Mei 2, 2026 dada wa Kareen, Elizabeth Didas, amesema mdogo wake alikuwa akiishi eneo la Shangarai, wilayani Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogo ndogo pamoja na masomo ya uhasibu kupitia Open University kwa njia ya mtandao.

Elizabeth amesema pia Kareen alikuwa na mipango ya kwenda nyumbani kwao Kahama, Shinyanga, kumtambulisha mchumba wake mfanyabiashara jijini Arusha baada ya kuhitimu mitihani yake ya mwaka wa kwanza wa masomo.

“Siku ya Jumatano Juni 18, 2025 tuliongea na Kareen mambo mengi ikiwamo maandalizi yake ya mitihani ya kuhitimu mwaka wa kwanza, lakini pia maandalizi ya kumtambulisha mchumba wake huyo nyumbani,

“Kiukweli alikuwa mwenye furaha kubwa akiniambia kuhusu pia maandalizi ya sherehe akidai mchumba wake amemwambia baada ya utambulisho wataunganisha, pamoja na mipango ya kulipa mahari na mipango ya kuoana,” amesema Elizabeth.

Elizabeth ameendelea kueleza kuwa siku mbili baadaye (Juni 20, 2025) alipokea simu kutoka kwa mdogo wake na baada ya kusalimiana, hakupata muda wa kuendelea kuzungumza naye kutokana na majukumu ya kazi.

“Najua mdogo wangu ana mazungumzo marefu, hivyo nilitaka anipigie jioni, nilidhani tutazungumza baadaye kama kawaida, lakini sikupata tena mawasiliano naye, kwani simu iliita bila kupokewa hadi leo.

“Ningejua anachotaka kusema si ajabu angeniambia hili na ningeweza kumshauri mdogo wangu, jambo zuri,” amesema Elizabeth na kuanza kulia.

Baada ya siku mbili za simu kuita bila kupokewa, Elizabeth amesema alipokea simu mchumba mtarajiwa wa mdogo wake, akimjulisha kuwa anajaribu kumtafuta Kareen bila mafanikio nilimjulisha pia mimi nampigia hapokei na sio kawaida yake.

Elizabeth amesema uchunguzi wa awali ulianza na kugundua kuwa usiku wa Juni 20, 2025 Kareen aliondoka nyumbani kwake Shangarai na kwenda Chuo cha Uhasibu kumchukua rafiki yake Nakivona, ili kwenda naye kwenye sherehe aliyodai ameandaliwa na mchumba wake huyo kumpongeza kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza.

Inadaiwa kuwa marafiki hao waliondoka pamoja usiku huo, tangu wakati huo hawajawahi kuonekana tena.

“Tatizo hatujui mdogo wangu yuko hai au amefariki, maana siyo kawaida yake kuwa kimya hivi, tunaomba jamani Serikali itusaidia kumpata mdogo wangu.

“Tunashuku kuna jambo kubwa linafichwa, hasa baada ya mchumba huyo anayedaiwa kuwachukua, kugoma kutoa ushirikiano kwa familia na mbaya zaidi amezima simu zake zote,” amesema.

Baba mdogo wa Nakivona, Kakai Daudi amesema msichana huyo ni yatima alikuwa akisoma Chuo cha Uhasibu Arusha akiwa katika hatua ya kumaliza cheti kabla ya kuendelea na diploma.

Amesema alipokea taarifa za kupotea kwa msichana wake Juni 23, 2025 na mara moja alisafiri hadi Arusha kufuatilia na kutoa taarifa polisi lakini hakuna matumaini.

“Tuligundua kuna mwanamume aliyewaalika kwenye sherehe ya usiku na baada ya kuhudhuria hawajarudi na hawakuonekana tena yeye na rafiki yake,” amesema.

Kakai amesema kuwa licha ya polisi kuahidi kufuatilia kesi hiyo, hadi sasa hakuna taarifa za matumaini zilizopatikana kwa binti yao wala mtuhumiwa kukamatwa.

“Tunaumia sana, maana inaonekana kuna mtu aliyekuwa na mawasiliano nao kabla ya kutoweka, lakini hakuna hatua za wazi zinazochukuliwa, zaidi tunabaki kuomboleza wakati mtuhumiwa yupo anaendelea na biashara zake,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa hana taarifa za ndani juu ya tukio hilo.

“Kama taarifa ilitolewa polisi na kufunguliwa jalada lazima linashughulikiwa. Kwa upande wangu sina taarifa za ndani kuhusu tukio hilo, naomba muda nifuatilie nijue ilipofikia kabla ya kutoa taarifa rasmi,” amesema Kamanda Masejo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *