Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahimiza wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika miradi mbalimbali, hususan ujenzi wa hoteli za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wageni, kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027.

Amesema serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana na wawekezaji, akisema fursa za uwekezaji ni kubwa kutokana na ujio wa mashindano hayo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado kuna uhaba wa miundombinu ya kisasa ya malazi yenye uwezo wa kupokea wageni wengi.

Chalamila alitoa kauli hiyo Mei 2,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya City Crown iliyopo mtaa wa Pemba na Lumumba, Kariakoo, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa maendeleo.

Amesema kuwa Tanzania imepewa heshima ya kuandaa AFCON 2027, hivyo ni muhimu kuongeza uwekezaji katika sekta ya hoteli ili kukidhi mahitaji ya wageni kutoka mataifa mbalimbali.

“Tatizo kubwa tulilonalo kwa sasa ni uhaba wa hoteli bora na za kisasa zitakazoweza kubeba wageni wengi watakaokuja kushuhudia mashindano hayo,” amesema.

Ameongeza uwepo wa hoteli ya City Crown ni kielelezo cha kukua kwa uwekezaji katika sekta hiyo, huku akieleza kuwa licha ya kuwepo kwa hoteli chache nzuri, bado mahitaji yanaendelea kuongezeka.

“Hoteli hii itakuwa kivutio kikubwa si tu kwa sekta ya utalii, bali pia ni ishara ya uwekezaji wa kisasa katika mkoa wetu wa Dar es Salaam,” amesema.

Akizungumzia uhusiano wa kimataifa, Chalamila amesema Tanzania na China ni marafiki wa muda mrefu, na ushirikiano wao umeendelea kuleta manufaa ya kidiplomasia na kiuchumi kwa pande zote.

“Uwekezaji huu ni alama na kielelezo kizuri cha urafiki uliodumu kwa miaka mingi. Ninafahamu kuwa ujenzi wa hoteli hii ulizingatia taratibu zote pamoja na ubora unaohitajika,” amesema.

Amewataka wawekezaji kuwa walipaji wazuri wa kodi ili kuchangia maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa mapato ya kodi huchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama barabara, umeme na huduma za kijamii.

“Kodi ikilipwa, taifa linaweza kujiendesha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi,” amesema.

Kuhusu ajira, Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza vijana wa Kitanzania kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na bidii.

“Nafahamu kuna changamoto ya uaminifu kwa baadhi ya vijana. Nawasisitiza vijana wote wanaopata ajira katika sekta hii kuwa mabalozi wazuri, jambo ambalo litachangia kuvutia uwekezaji zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Group Six, kampuni iliyojenga hoteli hiyo, Huang Zai Sheng, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Mazingira hayo yamechangia kufanikisha uwekezaji wa hoteli hiyo, ambao unaotarajiwa kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla,” amesema Sheng

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *