Dar es Salaam. Kampuni ya Bima ya CRDB Insurance imetangaza kupata faida baada ya kodi ya Sh4.4 bilioni kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2025, hatua inayoashiria mafanikio makubwa kifedha pamoja na utekelezaji madhubuti wa mikakati yake.

Kutokana na matokeo hayo, Bodi ya Wakurugenzi imependekeza kugawa gawio la Sh439 kwa kila hisa, sawa na jumla ya Sh1.5 bilioni, huku ikionesha matarajio chanya ya kuendelea kufanya vizuri zaidi katika mwaka 2026.

Katika kipindi hicho, kampuni ilikusanya michango ya bima yenye thamani ya Sh55.7 bilioni, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya kiasi kilichokusanywa mwaka uliotangulia.

Ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na huduma za bima ya magari, dhamana ya mikopo na bima ya moto, sambamba na mikakati imara ya usambazaji na kuongezeka kwa wigo wa soko.

Akizungumzia mafanikio hayo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Wilson Mnzava, amesema mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa uliodhihirisha ukuaji, uimara na utekelezaji thabiti wa mikakati ya biashara.

Amesema matokeo hayo yanaakisi uimara wa shughuli kuu za kampuni, ufanisi wa mifumo ya usambazaji pamoja na dhamira ya kutoa thamani kwa wateja.

Ameongeza kuwa kampuni imeimarisha uwezo wake wa utoaji huduma kwa kutumia teknolojia ili kuongeza ufanisi na kukidhi mahitaji ya wateja, huku ikijenga msingi wa kupata matokeo bora zaidi mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Mnzava, faida kabla ya kodi ilifikia Sh6.1 bilioni, huku thamani ya mali za kampuni ikiongezeka hadi Sh44.6 bilioni.

Aidha, amesema mtaji wa wanahisa umefikia Sh10.3 bilioni, hatua inayoonesha uimara wa kifedha na ukuaji endelevu wa kampuni.

“Teknolojia na ubunifu viliendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kampuni mwaka 2025 kupitia uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, uboreshaji wa michakato ya uandikishaji wa bima, ulipaji wa madai na shughuli nyingine za uendeshaji,” amesema. Inaelezwa kuwa hatua hizi zimeongeza kasi ya utoaji huduma na kuboresha ubora wa maamuzi ya biashara.

Kampuni pia imenufaika na mtandao mpana wa Benki ya CRDB kupitia huduma za bancassurance zinazotolewa kwa kutumia matawi, mawakala na majukwaa ya kidijitali, hali iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za bima kwa wateja wengi zaidi.

Sambamba na hilo, inaelezwa kuwa ushirikiano na madalali, mawakala na wateja wa taasisi umeendelea kuchochea ukuaji na utofauti wa biashara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Omary Mwaimu, amesema mafanikio hayo yanaonesha si tu ukuaji wa kampuni, bali pia ubora wa mifumo ya uongozi na usimamizi iliyopo.

Mwaimu amesema ongezeko la michango ya bima, faida na mtaji linaonesha ufanisi wa mkakati wa kampuni pamoja na nidhamu ya utekelezaji wake.

Hivyo, amesisitiza kuwa bodi itaendelea kuhakikisha kasi hiyo ya ukuaji inadumishwa huku ikilinda maslahi ya muda mrefu ya kampuni na wadau wake.

Mbali na pendekezo la gawio, bodi pia imeelekeza sehemu ya faida iliyopatikana kutumika kuimarisha mtaji na kusaidia mipango ya upanuzi wa biashara siku zijazo.

“Kampuni inawashukuru wateja, wanahisa, wadau, wadhibiti pamoja na wafanyakazi wake kwa kuendelea kuiamini na kuiunga mkono, jambo lililochangia mafanikio ya mwaka 2025 na kuimarisha matarajio ya kuendelea kufanya vizuri zaidi siku zijazo,” amesema Mwaimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *