
Kumekuwa na mijadala katika mitandao ya kijamii nchini, baadhi ya wachangiaji wakihoji hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Evaline Munisi kuingia katika baraza lake la mawaziri.
Wanaokosoa uamuzi huo wa Rais ni kama hawajaisoma vizuri Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayompa Rais mamlaka hayo au wanajisahaulisha kwa sababu Rais Samia sio Rais wa kwanza kumteua mpinzani.
Ukisoma Ibara ya 36(1) inasema bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba na sheria nyingine, Rais ana mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Tanzania.
Ibara ndogo ya (2) inampa Rais mamlaka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi.
Katika Ibara hizo, hakuna mahali popote panapompa Rais masharti kwamba asiteua mtu ambaye sio mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ndio maana hata waliomtangulia waliwahi kuteua watu kutoka upinzani.
Sasa Aprili 2, 2026, Rais Samia akitumia mamlaka yake halali kabisa ya Kikatiba, kwanza alimteua Munisi kuwa Mbunge wa Kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungani wa Tanzania na Mei 2, 2026 akamteua kuwa Naibu Waziri.
Munisi ambaye alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha NCCR Mageuzi Katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, anachukua nafasi ya Rahma Kisuo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Lakini tangu amteue mwanasiasa huyo kuwa mbunge wa kuteuliwa na baadaye Naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Uhusiano), kumekuwa na mijadala mizito mitandaoni utadhani Rais Samia kuna mahali amekosea.
Ukisoma Ibara ya 55(3) ya Katiba, inasema Rais anaweza kuteua idadi yoyote ya Naibu Mawaziri watakaowasaidia mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao na Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa miongoni mwa Wabunge.
Watanzania tujifunze kutokuwa na nongwa, kwa sababu Rais Samia sio Rais wa kwanza hapa Tanzania, kuteua mtu kutoka upinzani kushiriki katika shughuli za kujenga nchi, kwa sababu binafsi naamini kuwa mpinzani sio dhambi au uadui.
Vyama vya siasa ni daraja tu kwa sababu Katiba yetu imeweka sharti la lazima kuwa unapotaka kuwa mbunge chini ya Ibara ya 67(1)(b) ni lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa na adhaminiwe na chama hicho cha siasa.
Lakini tusisahau kuwa Katiba hii hii ya 1977 imesema wazi kuwa Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii tuliyonayo au na sheria nyingine yoyote.
Ni kutokana na mamlaka hayo, Mei 3, 2012, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete alimteua aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuwa Mbunge, akitumia Ibara ya 66(1)(e) ya Katiba ya Tanzania ya 1977.
Ibara aliyoitumia Kikwete kumteua Mbatia ndio hiyo hiyo ambayo Rais Samia ameitumia leo kumteua Munisi kuwa mbunge na baadaye Naibu Waziri.
Julai 16, 2016 Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alimteua mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu na 2020 akamteua tena kwenye nafasi hiyo.
Ni kwa mamlaka hayo hayo, Juni 3, 2017, Rais Magufuli ambaye baadaye alifariki dunia, alimteua Anna Mghwira kutoka Chama cha ACT -Wazalendo kuwa Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro. Baadaye mama Mghwira (marehemu) alijiunga na CCM.
Mei 15, 2021, Rais Samia akamteua Queen Sendiga aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) na mgombea urais kwa tiketi ya ADC kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na baadae akamhamishia Manyara.
Mimi nilitarajia uamuzi huu wa Rais kuwashirikisha hata walioko vyama vya upinzani katika kuijenga nchi yao ni jambo jema kuliko utamaduni uliozoeleka kuwa, ukiwa Rais unayetokana na CCM, basi uwachukulie upinzani kama maadui.
Ni kweli, kama vyama vyao vya upinzani vingeshika Dola basi vingetekeleza ilani ya vyama vyao na mipango ya maendeleo kwa miaka mitano, lakini kwa kuwa CCM ndio kiko madarakani, moja kwa moja wanakwenda kutekeleza ilani ya CCM.
Ninavyofahamu na ninadhani ndivyo itakavyotokea, hata Munisi hawezi kuendelea kubaki NCCR-Mageuzi, kwa vyovyote vile atavaa sare ya CCM ili afanane na wenzake, kama alivyofanya Mghwira na wengine.
Kama nilivyotangulia kusema, vyama vya siasa ni daraja tu la kufikia nafasi fulani ya kiasiasa, lakini kwa nafasi kama hizi za kisiasa kama Rais, wabunge na madiwani, inatakiwa mara anapochaguliwa anakuwa ni kiongozi wa wote.
Lakini ukisoma Ibara ya 13 (1) ya Katiba yetu hii ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 2000, inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Ukienda mbele zaidi na kusoma Ibara ndogo ya ((2) ya Katiba inasema ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.
Ibara ndogo ya (4) inazuia mtu yeyote kubaguliwa na mtu yeyote au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake na ikafafanua ubaguzi kuwa ni kumbagua mtu kwa utaifa wao, kabila, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini au jinsia.
Kwa hiyo mambo ya kubaguana kwa itikadi za vyama tunayaendekeza wenyewe na tunawapa nguvu watawala kutumia udhaifu huo kuwagawa watu ili kuwatawala kwa itikadi zao na imani zao za kisiasa, lakini Katiba haina sharti hilo la ubaguzi.
Ni kweli kunaweza kuwe na hisia kuwa hao wanaoteuliwa kutoka vyama vya upinzani kuingia katika nafasi hizi walikuwa ni mapindikizi au ni wasaliti na walikuwa na kazi maalum ndani ya upinzani, ukweli ni kuwa hizo ni hisia tu.
Lakini kama tumesahau kuwa Mei 7, 2021 miezi michache tu baada ya kurithi mikoba ya hayati Magufuli, Rais Samia aliwaahidi Watanzania kuwa ataingiza yeyote serikalini bila kujali huyu ametoka chama gani au yule katoka chama gani.
Labda niwarejeshe kwenye kile alichokisema wakati akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam ambacho ndio hiki anachokitekeleza sasa na wala si kigeni.
Rais Samia alisema katika kujenga uchumi wa Tanzania, kila Mtanzania anapaswa kuchangia bila kujali tofauti za kijinsia, rangi, kabila, dini au imani za kisiasa na akasema madhali ni Mtanzania, anastahili kushiriki katika ujenzi wa taifa hili.
Nikimnukuu alisema; “Huko mbele katika kupanga safu za kujenga uchumi, sitabagua yeyote. Mwenye weledi na umahiri anayeweza kuleta manufaa kwa Taifa nitamwingiza. Sitachagua huyu katika chama gani au yule katika chama gani.”
Kwa hiyo, Rais Samia kumteua Munisi ni kutimiza ahadi yake ya kutaka kuongoza Taifa lisilo na mgawanyiko unaotokana na itikadi za kisiasa, lakini kwa mjadala unaoendelea ni kama Watanzania tunatamani kubaguana kisiasa.
Tunapaswa kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi huu mgumu kwa sababu msifikiri wana CCM wote wanaojiona wao ni CCM kindakindaki na walikipigania chama hadi kushika madaraka wanafurahia hiki anachofanya Rais. Tumtie moyo.
Polepole twende kuifanya Tanzania kuwa ni yetu sote na kwamba, hakuna chama au mgombea mwenye haki miliki ya urais, ubunge au udiwani, bali yeyote anayeshinda bila kujali chama, achukuliwe kama ni mtanzania anaongoza.
Tukibadili fikira zetu na kujipeleka huko, nina hakika hata wale wana CCM waliotaka mabadiliko nao wataona ili Tanzania iwe salama, lazima tume na katiba mpya itakayowezesha uwepo wa taasisi imara na huru.
Ni kupitia Katiba iliyobeba maoni ya Watanzania, ndio itakayozaa Tume Huru ya Uchaguzi, Taasisi imara kama Bunge, Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ambazo zitafanya kazi kwa uhuru bila kupokea maagizo.
Kwa hiyo Watanzania tuache nongwa, Rais Samia sio wa kwanza.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900