Dar es Salaam. Ni takribani miaka 47 imepita tangu kuanguka kwa nguli wa muziki nchini, Mbaraka Mwinshehe.

Mbaraka aliacha sifa kubwa Ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na umahiri wake wa kuimba na kucharaza gitaa la solo, kutunga na kuongoza.

Kati ya sifa hizo zilizompa jina kubwa ni upigaji wa gitaa la solo, kipaji alichorithi mtoto wake, Muftaji ‘Taji’ Mbaraka Mwinshehe.

Licha ya kazi hiyo kuonekana ngumu hasa kwa wanawake, lakini Taji ameonyesha uwezo mkubwa tangu aanze muziki miaka ya 1990 akicharaza gitaa la bass ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitawaliwa na wanaume.

MWISH 03

Uwezo wake umewavutia mashabiki na wadau wa muziki kutokana na kupiga kitaa na kuimba kwa wakati mmoja na kudhihirisha ni mmoja wa vinara katika muziki wa dansi jukwaani.

Hadi sasa mchango wake umekubalika na kutunukiwa Tuzo ya Cheza Kidansi ya msimu wa saba ikiwa ni ishara ya kazi yake ya muda mrefu na mchango wake kwenye muziki wa jukwaani nchini.

Akiwa mmoja wa wanawake wachache wanaopiga gitaa la bass kwa umahiri, anaendelea kudhihirisha wanawake wana nafasi kubwa katika kuendeleza muziki wa bendi Tanzania.

MWISH 02

Tuzo ya cheza kidansi 

Taji hiyo imemfanya aongeze heshima kwenye jina la familia yake, kwa kuwa Mpiga Chombo Bora wa Kike katika tuzo hizo zilizofanyika Ijumaa, Mei Mosi, kwenye Ukumbi wa Ngoreme Park, Sinza, jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeendelea kuthibitisha mchango wake wa muda mrefu katika muziki wa jukwaani, huku akiendeleza kazi ya baba yake.

MWISH 04

Hamza Kalala amfungulia njia  

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwananchi, Taji anasema alianza safari ya muziki tangu miaka ya 90, akijifunza kwa bidii kabla ya kuingia rasmi kwenye bendi.

“Nilianza muziki mwaka 1990, nilikuwa naenda kujifunza kwa mwanamuziki mkongwe Hamza Kalala, baadaye nikawa naendelea kujifunza mwenyewe hadi nikajua zaidi. Muziki huu ndiyo maisha yangu, sana,” anasema na kuongeza, licha ya mwanzo kuwa mgumu, lakini aliwatumia wanamuziki waliomtangulia kujifunza .

Remmy Ongala anoa kipaji 

Anasema hatua muhimu katika maisha yake ya muziki ilikuja baada ya kushiriki tamasha la kumkumbuka baba yake lililofanyika Kinondoni miaka ya 90 na ndipo alipoonekana na kupewa nafasi ya kujiendeleza zaidi.

“Tulipofanya tamasha la kumkumbuka baba yangu, nilipoimba, Dr. Remmy Ongala akaniona na kuniambia nina kipaji kikubwa. Akanishauri niendelee na muziki na ndipo akanichukua kwenye bendi yake,” anaeleza.

Alikaa kwenye bendi hiyo kwa takribani miaka mitano, akijifunza muziki wa jukwaani na kujijengea uzoefu mkubwa.

MWISH 05

Aanzisha bendi

Baadaye alianzisha bendi yake ya Super Volcano, akiendeleza jina la bendi aliyoanzisha baba yake na alilazimika kujifunza kupiga gitaa la bass ili kukabiliana na changamoto za wapiga vyombo.

“Nilipenda sana kupiga gitaa la solo kama baba yangu, lakini wapiga bass walikuwa hawadumu. Nikasema bora nijifunze mwenyewe, nikaanza kupiga bass na kuimba kwa wakati mmoja,” anasema.

Baada ya ndoa na kupumzika kwa muda, Taji alirejea tena kwenye muziki akiwa msanii huru kabla ya kujiunga na Bahati Female Band, bendi ya wanawake pekee.

“Kwa sasa niko Bahati Female Band, tunaendelea na shoo na narekodi nyimbo za baba yangu ili ziendelee kusikika kwa kizazi hiki,” anasema.

MWISH 06

Akizungumzia ushindi wake, Taji anasema tuzo hiyo ni hatua kubwa kwa wanawake katika tasnia ya muziki, hasa wapiga vyombo ambao mara nyingi hawapewi nafasi kubwa.

“Nashukuru sana kwa kutambua wanawake kupitia kipengele hiki. Wanawake tuna uwezo mkubwa sana wa kupiga vyombo, lakini mara nyingi tunasahaulika. Hii imenipa moyo na naamini wengine watajitokeza zaidi,” anasema.

Alitoa wito kwa waandaaji wa tuzo nyingine kubwa nchini kuhakikisha wanaweka vipengele vya wapiga vyombo wanawake ili kukuza vipaji vilivyopo.

Kuedeleza kazi ya baba yake 

Mbali na maonyesho ya jukwaani, Taji anaendelea kurekodi na kuimba nyimbo za baba yake kama njia ya kuuenzi mchango wake katika muziki.

“Nimeamua kurudia nyimbo za baba yangu kwa sababu ni urithi wa familia na hakuna mtu mwingine wa karibu zaidi wa kuziendeleza. Nataka watu waendelee kuzikumbuka,” anasisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *