RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, tayari ameridhia na kutoa kiasi cha Dola za Marekani 30,000,000 (Sh78 milioni) kama ada ya uandaaji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hiyo ni ada ya uenyeji kwa AFCON 2027 ambazo hulipwa kwa shirikisho hilo na nchi mwenyeji au nchi wenyeji.

Kwa zabuni ya pamoja ya Afrika Mashariki ya mwaka 2027 ikizihusisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, kila nchi inapaswa kulilipa ada hiyo.

Gharama muhimu za kuomba na kuandaa AFCON mbali na ada ya uenyeji, pia kuna gharama za uendeshaji na inahusisha kuandaa mashindano, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya viwanja, hii inakadiriwa kufikia takribani Dola 104 milioni (Sh270.9 bilioni) kwa zabuni ya pamoja ya Afrika Mashariki.

MAKO 02

Pia uwekezaji wa miundombinu, matumizi halisi huwa makubwa zaidi kutokana na mahitaji yake. Kwa mfano, Senegal ilitumia zaidi ya Dola 1 bilioni kwa AFCON ya 2023, na Morocco kwa mwaka 2025 iliwekeza kwa kiwango kikubwa katika ukarabati wa viwanja.

Wakati huohuo, kulikuwa na ada ya awali ya kuwasilisha fomu ya maombi ya zabuni ambayo ni Dola 1,000 (Sh2.6 milioni).

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Paul Makonda alisema hii ndiyo tafsiri halisi ya Dk Samia Suluhu Hassan kama mwanamichezo namba moja nchini ambaye amedhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali katika kufanikisha mashindano ya AFCON 2027.

Makonda amethibitisha kuelekea mashindano ya AFCON 2027, wizara hiyo imejipanga kikamilifu kwa kushirikisha wadau wote kuhakikisha mashindano hayo sio tu yanafanyika bali yanaweka historia na alama isiyofutika nchini.

MAKO 03

Wakati huohuo, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kuwa ifikapo Agosti 2026, itakamilisha ukarabati wa miundombinu ya michezo katika miji wenyeji ya Dar es Salaam na Arusha kwa ajili ya AFCON 2027.

Makonda mwenye dhamani ya wizara hiyo, alisema ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 95, huku ukarabati wa viwanja vitatu vya mazoezi vya Gymkhana, Meja Jenerali Isamuhyo na Shule ya Sheria umekamilika. Pia ujenzi wa viwanja vitatu vingine vya mazoezi vya Farasi, Leaders Club na Gymkhana II vipo katika hatua za awali.

Alisema ujenzi wa Uwanja wa Arusha wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 32,000, umefikia asilimia 77.5 na ujenzi wa kiwanja kimoja cha mazoezi kinachojengwa katika eneo la Uwanja wa Arusha umefikia asilimia 60.

MAKO 01

Alisema, sambamba na maandalizi ya miundombinu ya AFCON 2027, Serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu mingine ya michezo nchini kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kukuza vipaji na kuboresha huduma za michezo kwa wananchi.

Aliitaja miradi mingine ambayo inatekelezwa ni ujenzi wa Akademi ya Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na utekelezaji wake umefikia asilimia 49, ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dodoma wenye uwezo wa kuchukua watu 32,500 ambao umefikia asilimia 5 sambamba na ujenzi wa Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 73.5.

Pia ujenzi wa Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi jijini Dar es Salaam kilichofikia asilimia 49 na ukarabati wa Uwanja wa Uhuru ambao umefikia asilimia 70.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *