Dar/Dodoma. Vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na ACT- Wazalendo ‘vimeungana’ katika hoja za upatikanaji wa Katiba mpya ili kulinda haki za binadamu, kuheshimu utawala bora na maridhiano.

Hata hivyo, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeibuka na kuzijibu hoja kikisema, Katiba mpya ni ajenda ya CCM na kupitia ilani yake ya 2025/30 iliahidi kufanya marekebisho.

Vikizungumza vyama hivyo kwa nyakati tofauti, vimedai kuwa mambo hayo ni lazima yafanyiwe kazi ili kuliponya Taifa na kuondoka kwenye mkwamo unaoliweka Taifa njia panda na kushindwa kupiga hatua ya kimaendeleo.

Baadhi ya hoja hizo kama ya Katiba mpya na maridhiano ni miongoni mwa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman.

Jaji Chande alipokabidhi ripoti hiyo Aprili 23, 2026, alisema wamependekeza Katiba mpya ipatikane kabla ya mwaka 2028 ikatumike katika uchaguzi mkuu wa 2030 na pia, maridhiano yafanyike; jambo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia na kuahidi kuunda kamati.

Wakati vyama hivyo vikieleza hivyo, jana Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema Katiba mpya ni ajenda ya CCM na kupitia ilani yake ya 2025/30 iliahidi kufanya marekebisho ya Katiba.

“Mgombea urais wa wakati huo ambaye kwa sasa ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa CCM katika mikutano yake ya hadhara alipokuwa anazungumza na Watanzania kuomba ridhaa alizungumza jambo hilo,” amesema.

Amesema katika chama hicho, Katiba mpya ni ajenda yao, huku akiendelea kuwahakikishia Watanzania kabla ya mwaka 2030 itakuwa imepatikana.

“Ikumbukwe chama kimekuwa kwenye mageuzi makubwa ya Katiba tangu mwaka 1977, mwaka 1984 Taifa lilifanya mabadiliko makubwa yaliyoimarisha haki za binadamu na kujenga misingi ya utawala bora,” amesema.

Amesema chama hicho kimefanya mageuzi hayo mara kwa mara na kitaendelea kufanya kwa kuzingatia matakwa ya nyakati zilizopo huku akisema tangu mwaka 1984 mchakato wa mabadiliko umekuwa ukifanyika hadi awamu ya nne na ilipitishwa sheria ya mabadiliko ya Katiba kuunda Bunge la Katiba na kupatikana Katiba pendekezwa.

“Mchakato wake ulikwama na waliokwamisha walikuwa vyama vya upinzani wenyewe kwa kususia mchakato huu, lakini CCM inaendelea kuhakikisha Katiba inayotakiwa inapatikana,” amesema.

Katika hoja hiyo ya Katiba, Kihongosi amesema wanaoidai wanapaswa kuelewa Katiba si mali ya vyama vya siasa bali ni mali ya Watanzania wote na ili kufikia hilo ni lazima wadau wote wahusishwe.

“Wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wasio na vyama ili kupata Katiba itakayokuwa na maoni ya wananchi wote kwa jumla, inashangaza kuona baadhi ya vyama vinapoongelea wanaangalia ajenda moja tu ya uchaguzi,” amesema Kihongosi.

Pia, amesema chama hicho kinaamini katika maridhiano kufanyika si mara ya kwanza kutokea nchini.

“Katika nyakati ambazo kelele na tofauti za kisiasa au kijamii na itikadi zinapoongezeka jambo moja la msingi kuliko yote ni hatima ya Taifa ambayo haiwezi kujengwa juu ya misimamo mikali bali kwa kukaa pamoja,”amesema Kihongosi.

Katika muktadha huo, Kihongosi amesema chama hicho kinatoa wito wa kushirikisha makundi yote vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, sekta binafsi viongozi wa kimila katika mazungumzo ya maridhiano.

“Kupitia falsafa ya Rais ya 4R imefungua dirisha la kihistoria mpya ambalo haliwezi kupuuzwa, sote tunakubali kuwa kukubali kuzungumza si ishara ya kushindwa bali ni ishara ya ukomavu wa kisiasa,” amesema Kihongosi.

Amesema mageuzi ya kweli hayazaliwi barabarani wala kwenye majukwaa ya kisiasa bali kwa kuketi kwenye meza ya mazungumzo ambako hoja hukutana na kuchambuliwa na hupatikana muafaka.

“CCM tunafahamu hata mataifa yaliyofanikiwa kujenga mifumo imara ya kisiasa na kiuchumi yamefanya hivyo, kwa kutathimini majadiliano wala si mashinikizo kutoka nje au kwa mtu yeyote,” amesema Kihongosi.

Pia, amefafanua hoja hiyo akisema kufanya hivyo aimaanishi kwamba wananchi hawana haki ya kudai mabadiliko la hasha! Lakini njia ya kufikia hilo lazima misingi ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa iheshimiwe.

“Kuna wenzetu, baadhi ya vyama ambavyo haviamini katika mazungumza bali vinaamini katika vurugu ambazo mwisho wa siku wanaenda kugharimu maisha ya watu wengine,”amesema Kihongosi.

Amesema nia ya siasa za kukamiana, kuonesha nguvu au kujenga mazingira ya hofu haiwezi kuwa mbadala wa mazungumzo yenye tija ingawa kwa muda mfupi inaweza kuonekana kama suluhisho.

“Niwaombe Watanzania tusikubali kupelekwa katika vurugu bali tukae na kujadiliana pamoja kama nchi, hivyo niombe viongozi wa siasa na wadau na wananchi kwa ujumla kuweza kushiriki pamoja ili kujenga Taifa imara,”amesema.

 “Kama viongozi wanapaswa kujitafakari na kujifunza mipaka ya demokrasia ambayo CCM imeendelea kuienzi na kuidumisha, mihimili ya nchi yetu iko mitatu, Bunge, Serikali na Mahakama na tunajua kila chombo kinafanya kazi kwa utashi wake bila kuingiliwa,”amesema Kihongosi.

Hoja za upinzani

Akiwasilisha maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema dai la Katiba mpya ni la muda mrefu, hivyo kamati kuu ya chama hicho inaona Watanzania hawawezi kusubiri tena mchakato isipokuwa hivi sasa.

“Kwa sababu hiyo, kamati kuu imeazimia kuundwa kwa kamati ndogo ya kamati kuu ili kuandaa mkakati wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya.

“Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa muswada wa kisheria kwa niaba ya wananchi utakaoeleza utaratibu wa kukwamua, kuendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya,”amesema Mnyika.

Upande wa ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita amesema kamati kuu ya chama hicho imeazimia mchakato wa Katiba mpya kwa kuanza na hatua kadhaa ikiwamo kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho ya Sheria ya Katiba.

“Uitishwe mkutano wa kitaifa utakaoshirikisha wadau wote nchini ili kupata muafaka wa masuala ya juu ya Katiba ambayo ni nyeti na hayana muafaka ikiwamo muundo wa muungano,” amesema Mchinjita.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf amesema wanaiunga mkono hoja ya maridhiano, akieleza kwamba masuala yanayoibuliwa na vyama vingine ni yale ambayo wao wamekuwa wakiyasisitiza kwa muda mrefu.

“Ni madai yetu ya muda mrefu kuhusu Katiba mpya, na hata watangulizi wangu walikuwa wakizungumza hoja hiyo kwa kipindi kirefu, lakini haijawahi kupatiwa majibu,” amesema Yusuf.

Amesema wanathamini hoja ya maridhiano na tayari wameanza kuitekeleza ndani ya chama chao.

“Tumeanza kuifanya hata ndani ya chama chetu kwa kuwapa nafasi wanachama wote wenye malalamiko kueleza yaliyo moyoni, ili tujenge umoja na kuimarisha chama kwa pamoja,” amesema Yusuf.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *