Dar es Salaam. Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa (Pathologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Angela Mwakimonga, amesema imani potofu kuhusu ugonjwa wa saratani ni janga linalosumbua kwa sasa.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni, daktari huyo amesema wanapokea baadhi ya wagonjwa wanaogoma kukatwa kinyama kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, wakidai kufanya hivyo kunaweza kusambaza zaidi ugonjwa.

“Ili daktari bingwa ‘pathologist’ aweze kukuambia wewe una ugonjwa gani, ni lazima kinyama kikatwe, tunaita ‘biopsy’. Baada ya kupima ndipo tunakutana na majibu kama una saratani au la.

“Kwahiyo mtu akikwambia usifanye hiyo ni upotoshaji, kwa sababu huwezi kujua mtu ana ugonjwa gani bila kufanya biopsy. Hakuna utafiti unaoonesha kwamba ukataji wa nyama kwenye uvimbe unasababisha usambae,” amesema.

Angela amesema wapo baadhi ya watu wanaopotosha na kuleta taharuki kwa jamii.

“Tunapata changamoto sana, mgonjwa akija kufanya uchunguzi anaogopa. Anasema ameambiwa itasambaa, inahitaji jamii ijue kwamba si sawa, ni dhana potofu.

“Miaka yote kukata kinyama na kukichunguza ndiyo kiwango bora cha utambuzi wa ugonjwa. Ndicho tunachokitegemea mpaka leo kutuambia mtu ana ugonjwa gani,” amesema Angela.

Aidha, daktari huyo amesema ugonjwa wa saratani bado ni janga huku akitaja aina za saratani  zinazosumbua.

“Kuna ya shingo ya kizazi, ya matiti na hata saratani ya tezi dume. Sasa hata ya tumbo inakuja juu.

“Zipo saratani hata kwa watoto na mara nyingi zinatokana na jenetiksi. Ulaji wa mama wakati wa ujauzito hauhusiki. Hata kama wazazi wake hawana, mtoto anaweza kupata,” amesema Angela.

Daktari huyo bingwa wa uchunguzi amesema kazi yao kubwa ni kugundua saratani.

“Huko mtaani kuna watu wana viuvimbe mbalimbali au kitu ambacho anaona ni kigeni mwilini, sisi kazi yetu ni kukichunguza hicho kitu na kugundua ni aina gani ya ugonjwa.

“Kazi yetu pia hata kwenda mtaani kuzungumza na watu, kuwaeleza namna wanavyoweza kufanya uchunguzi mara kwa mara kabla magonjwa hayajafika mwisho na kuleta madhara.

“Yapo magonjwa mengi lakini nitazungumzia saratani. Kwanza inatibika ikiwahiwa, na inazuilika ukiwahi na kufanya uchunguzi mara kwa mara,” amesema na kuongeza kuwa;

“Mfano saratani kwenye shingo ya kizazi, wanawake wakifanya uchunguzi mapema wanaweza kugundua viashiria na ikatibika kabla ya kukufikisha kwenye umauti.”

Kutokana na tabia ya baadhi ya watu kutopenda kufanya uchunguzi wa miili yao mara kwa mara, Angela amesema hujikuta wakigundua wanaumwa wakiwa wamechelewa.

“Kwa bahati mbaya watu wengi wanakuja wakiwa hatua za mwisho. Kuna dhana nyingi mtaani, ukiwauliza wengine wanasema walikuwa kwa mganga au wachungaji, hadi anarudia ugonjwa unakuwa umesambaa. Kama wangewahi ingekuwa rahisi,” amesema Angela.

Ametoa rai kwa jamii kushtuka kila wanapoona vitu visivyo vya kawaida kwenye miili yao.

“Kuna magonjwa mengine kama mtu hajaenda haja kubwa mwezi, unatakiwa kushtuka, hutakiwi kuchukulia kawaida. Kwa sababu unatakiwa kupata haja kila siku.

“Kuna vitu viko wazi, ukiona kitu kimebadilika, shtuka. Hata kwenye matiti unaweza kujishika na ukagundua, ukiona vitu vimejitokeza sio vya kawaida, shtuka. Bila kusahau viuvimbe kwenye mwili,” amesema.

Amesema watu hawapaswi kuwa na uoga, badala yake wafuatilie kila kitu katika miili yao.

“Kuna magonjwa mengi yanayosumbua watu. Hata hiyo tezi dume, sio kila tezi dume ni kansa, zipo ambazo zimevimba tu. Kuna uvimbe mwingine kwenye ziwa ambao sio kansa, kwa hiyo ukifuatilia utajua mapema kinachokusumbua,” amesema.

Ikumbukwe Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ilizitaja aina 10 za saratani zinazosumbua katika Mkoa wa Dar es Salaam, huku saratani ya utumbo ikitajwa kuongoza kwa wanaume na kwa wanawake ni saratani ya mlango wa kizazi.

Takwimu hizo zilitajwa Februari 4, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo, alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, katika maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani.

Takwimu za kanzi data ya saratani kwa Dar es Salaam kwa mwaka 2023 zinaonesha aina za saratani zinazoongoza kwa wanaume ni saratani ya utumbo asilimia 18.4, saratani ya koo la chakula asilimia 12, saratani ya ini asilimia 10.1, saratani ya tezi dume asilimia 10, pamoja na saratani ya mapafu kwa asilimia 8.

Kwa upande wa wanawake, aina za saratani zinazoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 18.2, saratani ya utumbo asilimia 15.1, saratani ya matiti asilimia 12.6, saratani ya ini asilimia 11.8, na saratani ya koo asilimia 5.7.

Ameendelea kusisitiza kuwa magonjwa mengi yanasababishwa na mfumo wa maisha ambao watu wanaishi.

“Mfano kupunguza mwili au kunenepa ni diet sana sana. Kuliko kutumia vitu vya kukuongeza au kukupunguza, ni heri mtu abebe chuma na kupunguza wanga, utakuwa na hiyo six pack ambazo watu wanatafuta,” amesema.

Aidha, katika hotuba iliyosomwa na aliyekuwa Waziri wa Afya Juni 2025, Jenista Mhagama, ilieleza kuwa saratani ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayopewa kipaumbele nchini.

Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya wagonjwa wapya wa saratani 11,801 waligunduliwa na kuanza matibabu katika hospitali mbalimbali za rufaa.

“Serikali imewekeza katika huduma za uchunguzi na matibabu, ikiwemo ununuzi wa mashine ya PET CT-Scan yenye thamani ya shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya uchunguzi na ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani.

“Pia, huduma za tiba mionzi zimeimarishwa, ambapo wagonjwa 152,287 walipatiwa tiba hiyo. Aidha, ujenzi wa jengo la huduma za tiba mionzi katika KCMC unatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi Juni 2025,” alisema katika hotuba hiyo na kuongezea;

“Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ambapo watu milioni 20 walifikishwa na elimu hiyo katika kipindi hicho,” alisema.

Mfumo wa maisha tatizo

Akizungumzia matumizi ya Akili Mnemba kwenye sekta ya afya, amesema kwa upande wake bado haijamvutia.

“AI inakupa kila kitu lakini kwenye afya mimi sipendi matumizi ya AI, kwa sababu unakutana na mtu ana kwa ana na unatakiwa kumhudumia.

“Nafikiri mtu anatakiwa kusoma sana ugonjwa, kuona na kufanya, ndio inakuwa perfect kuliko kutegemea AI kwenye kila kitu,” amesema.

Amesema ili kupata wataalamu wengi katika sekta ya afya, jitihada kubwa ziendelee kuwekwa kwenye elimu ya sayansi.

“Pia inatakiwa wazazi kuwasaidia watoto, kuwaambia hakuna wanachoweza kushindwa, ili waweze kupata ujasiri wa kuingia kwenye sayansi, kwani kizazi cha sasa kinatakiwa kupewa moyo zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *