Maafisa wa serikali ya Marekani wamesema kwamba maajenti wa Huduma za Siri (Secret Service) wamempiga risasi na kumjeruhi mwanaume aliyekuwa na silaha katikati mwa jiji la Washington, D.C., karibu na Mnara wa Washington siku ya Jumanne, na kusababisha kufungwa kwa muda Ikulu ya White House.

Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Siri, Matthew Quinn, ametangaza kwamba ufyatuaji risasi huo ulitokea karibu na Jumba la Taifa muda mfupi baada ya msafara wa Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance kupita eneo hilo.

Amewaambia waandishi wa habari kwamba haamini kuwa makamu wa rais ndiye aliyelengwa, wala hajui kama tukio hilo lilihusiana na majaribio ya hivi karibuni ya mauaji dhidi ya Rais Donald Trump.

“Sitakisia kuhusu suala hilo,” ameeleza Matthew Quinn na kuongeza kuwa: “Sijui kama ufyatuaji risasi huo ulimlenga rais au la, lakini tutaweka wazi jambo hilo.”

Quinn amesema kwamba ufyatuaji risasi huo ulitokea baada ya maafisa wa Idara ya Usalama kumuona “mtu aliyeshukiwa” ambaye alionekana kuwa amebeba bunduki.

Amesema mwanamume huyo alikimbia kwa miguu baada ya maafisa kumkaribia, kisha akatoa silaha na kufyatua risasi.

Aliongeza kuwa maafisa wa Secret Service walijibu kwa risasi na kumjeruhi. Mpitanjia aliyekuwa karibu na eneo hilo pia alipatwa na majeraha madogo wakati wa tukio hilo.

Tukio hili linakuja karibu wiki moja baada ya mtu aliyekuwa na silaha kujaribu kuvamia hoteli moja mjini Washington ambapo Trump alikuwa akihudhuria dhifa ya Chama cha Waandishi wa Habari cha Ikulu ya White House.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *