MJADALA ukiwa unaendelea chini kwa chini wa viongozi wa Simba kutaka kuachana na kipa Djibrilla Kassali, anayehusishwa kuchukua nafasi yake ni golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Nigeria, Stanley Nwabali ambapo mwenyewe ametoa neno akibainisha kwamba, hana shida yoyote kuja Tanzania kucheza.

Ipo hivi; Baada ya Mwanaspoti kuripoti uwepo wa mazungumzo baina ya viongozi wa Simba na Nwabali ambaye aliwahi kuichezea Chippa United ya Afrika Kusini, gazeti hili limezungumza na kipa huyo ambaye pia anahusishwa na Azam inayotaka huduma yake kama mbadala wa Issa Fofana ikielezwa mwasho wa msimu huu inaweza kuachana naye.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nwabali alisema: “Kucheza Ligi ya Tanzania sioni shida, kwa sababu navutiwa zaidi kwa namna timu zinazopata nafasi za kushiriki michuano ya CAF zinavyoonyesha ushindani mkubwa.

“Nina marafiki wengi wanaocheza ukanda huo wa Afrika Mashariki, jambo la msingi kwa timu inayonihitaji huduma yangu ni kufikia makubaliano ya kimasilahi.”

Kitendo cha Simba kwenda kuzungumza na Nwabali ni kutokana na changamoto ya magolikipa wao kupitia kipindi cha majeraha, ambapo aliyekuwa namba moja, Moussa Camara, alitolewa kwenye mfumo wa usajili ili kumpa muda wa kujiuguza, ndipo akasajiliwa Kassali.

Camara aliyemaliza kinara wa cleansheets 19 msimu wa 2024-2025 ndani ya Ligi Kuu Bara, kwa sasa anaonekana kufanya mazoezi na viongozi walikuwa wanaangalia maendeleo yake kama watamrejesha katika mfumo kwa msimu wa 2026-2027 pamoja na hayo yote vigogo wa Wanamsimbazi wanajihami kutafuta mwingine kama mambo hayataenda sawa.

Kipa mwingine wa timu hiyo na Taifa Stars, Yakoub Suleiman aliyekuwa ameumia akiwa na timu ya taifa nchini Morocco wakati ikijiandaa kucheza na Nageria mechi ya Afcon 2025, kwa sasa kuna taarifa za afya yake inaimarika na huenda mechi za mwishoni anaweza akapata nafasi ya kucheza, itategemeana na mahitaji ya kocha.

Kabla ya kuachana na Chippa United Februari 1, 2026, Nwabali alicheza mechi 12, ambapo 11 za Ligi Kuu ya Afrika Kusini akiruhusu mabao 16, huku mechi tatu akitoka bila ya kuruhusu bao. Mechi nyingine aliyocheza ni Kombe la Carling Knockout.

Akiwa na timu ya taifa ya Nigeria, Nwabali ameonyesha uzoefu mkubwa katika mechi za kimataifa akicheza jumla ya mechi 34, kati ya hizo sita hajaruhusu bao huku akiruhusu mabao 29.

Wastani wa mabao anayoruhusu uko chini ya bao moja kwa kila mechi (takriban 0.85), hali inayomuweka katika kiwango kizuri ukilinganisha na makipa wengi wa kimataifa. Ingawa idadi ya clean sheets ni sita pekee kati ya mechi 34.

Mwanaspoti liliandika kwamba Nwabali aliipa Simba masharti ili asaini ambapo mshahara kwa mwezi ni Dola 15,000 (Sh39 milioni) sawa na ongezeko la asilimia 25 ya mshahara aliokuwa anaupata akiwa Chippa United, ambako ilikuwa Dola 12,000 (Sh31.2 milioni).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *