SARE ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, imeiacha Yanga kwenye maumivu makubwa, baada ya kukosa Sh1 bilioni ambayo wachezaji walikuwa wameahidiwa na tajiri wa klabu hiyo endapo wangeibuka na ushindi katika dabi hiyo iliyokuwa na presha kubwa.
Inaelezwa, kabla ya mchezo huo, wachezaji wa Yanga walipewa ahadi ya fedha hizo ikiwa ni motisha ya kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Simba, jambo lililoongeza morali na ari ya kupambana uwanjani.
Hata hivyo, matokeo ya sare yamewafanya wabaki na majuto, wakiamini walikuwa na kila sababu ya kushinda mchezo huo.
Mmoja kati ya wachezaji wa kikosi cha Yanga, aliliambia Mwanaspoti:
“Ulikuwa mchezo muhimu sana kwetu, si tu kwa heshima ya dabi bali hata hii ahadi ya fedha. Wachezaji walipambana kwa nguvu zote wakiamini ushindi unawezekana, ndio maana hata walipokuwa nyuma walirudi na kusawazisha, lakini bahati haikuwa upande wetu.”
Hata hivyo, katika kujaribu kuwainua kisaikolojia wachezaji wao, mabosi wa Yanga wameanza mipango ya kuwapa kiasi kidogo ya kile walichoahidiwa wakitambua juhudi kubwa iliyoonyeshwa na kikosi hicho hasa kupambana hadi kurejea mchezoni.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema:
“Viongozi tunatambua mchango wa wachezaji kwenye mchezo ule, wanajua walijituma sana. Kuna mpango wa kuwapa kiasi fulani ili kuwapa morali ya kuendelea kupambana kwenye mechi zijazo.”
Wakati Yanga wakiumizwa na kupoteza nafasi ya kuvuna kiasi hicho cha fedha, upande wa Simba nao ulikuwa na motisha yao ambapo inaelezwa waliweka mezani Sh500 milioni, wakilenga kuhakikisha wanapata ushindi katika dabi hiyo.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Simba kuikosesha Yanga vibunda kwani dabi iliyopita katika fainali ya Kombe la Muungano ambayo kama wangeshinda wangevuna Sh300 milioni, lakini wakafungwa 1-0.
Simba yenyewe iliposhinda dabi hiyo na kuwa bingwa wa Kombe la Muunga, iliondoka na jumla ya Sh450 milioni ambapo Sh150 milioni za ubingwa, na Sh300 milioni kutoka kwa viongozi kama sehemu ya bonasi.