WAKATI Kajuna FC na Kahama Madini zikipanda First League, Rhino Rangers na Bandari zimefuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu ujao baada ya kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani.

Bandari FC iliyopo kundi A, inaongoza kwenye msimamo kwa pointi 29 ikiwa na michezo miwili mkononi, ikifuatiwa na Nyumbu yenye pointi 23 ikipapatuana na Cosmopolitan yenye 22 na kila timu inasubiri dakika 180 kujua hatma yake.

Katika kundi hilo, timu za Pan Africa iliyopo mkiani kwa pointi 9, Green Worriors (11) na Dar City (11), zinachuana vikali kukwepa kushuka daraja moja kwa moja zikiomba huruma ya kuangukia play off au kubaki salama katika ligi hiyo.

Kwa upande wa Rhino Rangers, ndio vinara wa kundi B kwa pointi 31 wakiwa bado na mechi mbili kumaliza msimu, ambapo kwa hali hiyo haiwezi kufikiwa na timu yoyote katika kundi hilo na kujihakikishia kucheza Ligi ya Championship msimu ujao.

Maafande hao wa mkoani Tabora waliowahi kushiriki Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja msimu wa 2014-2015, wamerejea Ligi ya Championship baada ya kudumu kwa misimu minne na sasa wanaisaka tena Ligi Kuu.

Katika kundi hilo, tayari Biashara United wameshuka daraja huku Mapinduzi na Copco zote za jijini Mwanza zenye pointi 14, zikipapatuana kukwepa kushuka daraja ilhali IAA (pointi 24) na Endument (pointi 20) zikisaka kupanda kupitia play off.

Mtendaji Mkuu wa Bandari FC, Ismail Chimpele, alisema mafanikio hayo si ya mtu mmoja bali ni ushirikiano wa pamoja na kwamba kwa sasa wanajiwinda na mechi mbili za mwisho kumaliza kibabe.

Kimsingi tunashukuru ushirikiano na sapoti kubwa ya uongozi chini ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa bandari, baada ya ligi kuisha tutaanza mipango mipya ya Championship,  alisema Ismail.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *