Wafungwa kumi na mmoja wa Tunisia wameyataka makundi ya upinzani nchini humo “kuungana ili kurejesha uhuru na demokrasia” nchini humo.

Wito huo umetolewa katika barua iliyosainiwa na wafungwa wa kisiasa walioshtakiwa katika kesi zinazohusiana na “njama dhidi ya usalama wa taifa.

Orodha ya waliotia saini ni pamoja na mkuu wa “National Salvation Front (FSN)” Ahmed Nejib Chebbi, mwanachama wa kundi hilo Jawhar Ben Mbarek, waziri wa zamani Ayachi Hammami, kiongozi wa Harakati ya Ennahdha, Rached Ghannouchi, Katibu Mkuu wa Chama cha Republican Issam Chebbi, na kiongozi wa zamani wa Ennahdha, Abdelhamid Jelassi.

Waliotia saini barua hiyo, ambayo imechapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Ghannouchi, wamesema kwamba Tunisia “inapitia awamu nyeti katika historia yake,” ikizingatiwa kwamba hatua za Rais Kais Saied mnamo Julai 25, 2021, ziliathiri “mafanikio ya mapinduzi na mpito wa kidemokrasia.”

Tunisia umekumbwa na mgogoro wa kisiasa tangu Julai 25, 2021, wakati Rais Kais Saied alipotangaza hatua za kipekee zilizojumuisha kuvunja Bunge na kubadilisha Katiba, hatua ambazo upinzani unasema ni “mapinduzi dhidi ya Katiba.”

Wafungwa wa kisiasa waliosaini barua hiyo wamesema: “Leo, Tunisia imerejea katika hali ya dhulma na utawala wa kidikteta, jambo ambalo linafanya juhudi za kurejesha mafanikio ya mpito wa kidemokrasia kuwa kazi ya pamoja ya wademokrasia wote, na jukumu kuu la kipindi cha sasa cha kihistoria.”

Wameongeza kuwa: “Kwa hivyo, wafungwa wa kisiasa waliosaini hapa chini, kutoka mirengo mbalimbali ya kifikra na kisiasa, wanawaomba wenzao wa harakati za kidemokrasia na asasi za kiraia kuungana na kufanya kazi pamoja ili kurejesha uhuru na kufufua demokrasia, kama njia ya kuelekea kwenye heshima na uhuru wa Tunisia.”

Mamlaka ya Tunisia hapo awali iliwakamata wanasiasa na wanaharakati kadhaa katika kesi tofauti, ikiwa ni pamoja na ile inayojulikana kama “njama dhidi ya usalama wa taifa,” ambayo ilijumuisha viongozi wa upinzani, ikiwa ni pamoja na viongozi wa National Salvation Front na Harakati ya Ennahda.

Upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kukamatwa huku ni ukandamizaji dhidi ya uhuru na shughuli za kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *