USHINDI wa Yanga wa bao 1-0 dhidi ya KMC, umeacha gumzo kwa mashabiki, sio tu kwa matokeo bali pia uamuzi wa benchi la ufundi la timu hiyo yaliyobadili mwelekeo wa mchezo huo.

Yanga imeifunga KMC bao 1-0 kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Allan Okello dakika ya 65 akimalizia pasi ya Shekhan Khamis, mechi iliyochezwa leo Mei 6, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.

Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa na ladha tofauti kipindi cha pili, baada ya mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na kocha wa Yanga, Pedro Goncalves.

Dakika ya 62, kocha huyo alifanya uamuzi ulioibua mjadala mkubwa uwanjani kwa kumtoa beki wa kulia, Yao Attohoula na kumuingiza winga, Buba Jammeh.

Mabadiliko hayo hayakuwafurahisha baadhi ya mashabiki wa Yanga waliokuwa uwanjani, huku wakionekana wazi kupinga kwa kusimama na kutoa ishara za kutoridhika.

Hali hiyo ilichangiwa na ukweli kuwa Yao alikuwa akionyesha kiwango kizuri, akisaidia timu kushambulia na wakati huo huo kuimarisha safu ya ulinzi.

Ndani ya dakika 62 alizocheza, beki huyo alionekana kuwa na mchango mkubwa, jambo lililowafanya mashabiki wengi kuona hakukuwa na ulazima wa kumtoa.

Baadhi yao walisikika wakieleza kuwa tangu arejee kutoka majeraha, Yao amekuwa katika kiwango kizuri hasa kwenye mechi za Kombe la Muungano.

Hata hivyo, benchi la ufundi lilionekana kuwa na mpango wake, ambapo mabadiliko hayo yalilenga kuongeza nguvu ya ushambuliaji kwani winga Max Nzengeli alichukua nafasi ya Yao kwenye ulinzi, na Buba alisogea juu kwenye nafasi ya Nzengeli.

Dakika chache baadaye, Yanga iliendelea kufanya mabadiliko mengine, ambapo Aziz Andabwile alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Shekhan Khamis.

Dakika ya 65, mabadiliko yalianza kuonekana, baada ya Allan Okello kufunga bao hilo pekee lililoipa pointi tatu Yanga.

Bao hilo liliamsha shangwe uwanjani na kuwanyamazisha kwa kiasi mashabiki waliokuwa na hasira kufuatia mabadiliko ya awali.

Pia, Okello alitoka na kuingia Salum Abubakar ‘Sure Boy’, mabadiliko yaliyoonyesha wazi kocha alikuwa akitafuta muundo bora wa kupata bao.

Ushindi huo una maana kubwa kwa Yanga katika mbio za ubingwa, kwani umeongeza gepu la pointi dhidi ya wapinzani wao Simba ambao wanacheza na JKT Tanzania.

Kwa sasa Yanga inaongoza ligi na pointi 51 baada ya mechi 21, huku Simba kabla ya kukabiliana na JKT Tanzania, ilikuwa na pointi 43 sawa na Azam zikiachwa pointi nane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *