
Ugonjwa wa kisukari umeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii, huku wataalamu wakionya kuwa unaweza kusababisha kifo cha ghafla, hata wakati mtu akiwa amelala.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya watu wanaoishi na kisukari nchini inaongezeka kwa kasi, ikikadiriwa kufikia zaidi ya watu milioni 2.9, huku wengi wao wakiwa hawajagundulika mapema.
Kwa kiwango cha dunia, takribani asilimia 14 ya watu wazima wanaishi na ugonjwa huo, wakati nchini Tanzania unaathiri karibu asilimia 9.8 ya watu wazima, idadi inayokaribia wastani wa kimataifa.
Utafiti mwingi unaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo kisukari, yanachangia takribani asilimia 33 ya vifo vyote nchini, jambo linaloashiria uzito wa tatizo hili.
Kisukari ni ugonjwa sugu unaotokea pale mwili unaposhindwa kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu.
Ingawa sukari ni chanzo muhimu cha nishati, kiwango chake kisipodhibitiwa huweza kusababisha madhara makubwa kama magonjwa ya moyo, kiharusi na kushindwa kwa figo.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani yaliyofanyika Novemba 2025, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, kisukari na homoni kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Dk Sania Kasiandu, alisema sababu za kisukari hutofautiana kulingana na aina yake.
Alifafanua kuwa kisukari aina ya kwanza hutokana na mfumo wa kinga kushambulia kongosho na kuzuia uzalishaji wa insulini, wakati aina ya pili husababishwa zaidi na mtindo wa maisha usiofaa, ikiwamo lishe duni, kutofanya mazoezi na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Hatari ya kifo cha ghafla usingizini
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kisukari kinaweza kusababisha kifo cha ghafla usingizini, hasa pale ugonjwa unapokuwa haujadhibitiwa ipasavyo.
Moja ya sababu kuu ni kushuka kwa sukari kupita kiasi (Hypoglycemia). Hali hii hutokea pale kiwango cha sukari kinaposhuka chini ya kawaida na kusababisha ubongo kukosa nishati.
“Endapo mgonjwa atapata hypoglycemia akiwa amelala, anaweza kushindwa kugundua dalili na kupoteza fahamu, hali inayoweza kusababisha kifo ikiwa hatapata msaada wa haraka,” anaeleza Dk John Mhando.
Anaongeza kuwa wakati wa usiku ni vigumu kwa mgonjwa kutambua dalili kama kutetemeka au njaa. Sukari ikishuka sana, ubongo hukosa nguvu, mgonjwa hupoteza fahamu na hatimaye kufariki akiwa usingizini, hali inayotokea zaidi kwa wanaotumia insulini au dawa kali za kisukari.
Kwa upande mwingine, kupanda kwa sukari kupita kiasi pia ni hatari. Hali hii inaweza kusababisha matatizo kama mwili kukosa maji, damu kuwa nzito na viungo kushindwa kufanya kazi vizuri. Bila matibabu ya haraka, hali hizi zinaweza kusababisha kifo, hata wakati wa usingizi.
Aidha, wagonjwa wa kisukari wako kwenye hatari kubwa ya matatizo ya moyo, ikiwamo mshtuko wa moyo na mapigo yasiyo ya kawaida ya moyo. Kisukari huathiri mishipa ya damu na kuongeza uwezekano wa matatizo haya kutokea ghafla, mara nyingi bila dalili za awali.
Muuguzi Mkuu kutoka Hospitali ya Qualitas Kigamboni, Priscus Kilawe, anasema mabadiliko ya ghafla ya sukari mwilini iwe kupanda au kushuka, yanaweza kusababisha kifo.
“Sukari ikishuka sana, mwili hukosa nishati ya kufanya kazi. Mfano ukiwa na kiwango cha chini sana, mgonjwa anaweza kupoteza fahamu na kufariki. Wakati mwingine hutokea bila dalili za wazi, hasa akiwa amelala,” anafafanua.
Anaongeza kuwa kupanda kwa sukari kunaweza kuathiri viungo muhimu kama figo na ini, pamoja na kuvuruga uwiano wa madini mwilini, hali inayoweza kusababisha kifo ikiwa haitadhibitiwa mapema.
Ushuhuda na tahadhari kwa wagonjwa
Baadhi ya wagonjwa wameelezea uzoefu wao kuhusu hatari ya kisukari, hususan wakati wa usiku.
Olivera Antony ambaye anaishi na kisukari kwa muda mrefu, anasema amewahi kunusurika mara kadhaa kufariki kutokana na kushuka kwa sukari akiwa amelala.
“Wakati mwingine napoteza fahamu kabisa, siwezi kuongea wala kuomba msaada. Mwili unakuwa hauna nguvu, viungo vinakakamaa na hubaki macho pekee. Watoto wangu hunisaidia kwa kunipa huduma ya kwanza na kunikimbiza hospitali,” anasimulia.
Kwa upande wake, Asnat Juma, mkazi wa Gongo la Mboto, anasema alimpoteza baba yake aliyekuwa na kisukari baada ya kufariki ghafla usingizini bila dalili za awali.
Wataalamu wanasisitiza kuwa hali hii inaweza kuzuilika kwa kufuata ushauri wa kitabibu. Miongoni mwa mambo muhimu ni kupima sukari mara kwa mara, hasa kabla ya kulala, kula lishe sahihi, kufuata dozi za dawa, na kuepuka pombe kupita kiasi.
Dalili za tahadhari za kushuka kwa sukari ni pamoja na kutetemeka, kutoka jasho jingi, mapigo ya moyo kwenda kasi, kizunguzungu, njaa kali na kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu
Mtu anapohisi dalili hizi anapaswa kula au kunywa kitu chenye sukari haraka, kama juisi au pipi, na kufuatilia hali yake.
Aidha, familia zinazowahudumia wagonjwa zinapaswa kuwa na uelewa wa dalili hizi na namna ya kutoa msaada wa haraka, hasa nyakati za usiku ambapo mgonjwa hawezi kujisaidia mwenyewe.