
Gazeti la Kiebrania Ma’ariv limeripoti kwamba Lebanon imekuwa kinamasi cha misukosuko na mawimbi makali, chenye gharama kubwa kwa Israel.
Ni baada ya vyanzo vya Kiebrania kuripoti Ijumaa shambulizi hatari kusini mwa Lebanon dhidi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na operesheni za kuhamisha askari waliojeruhiwa na hata maiti za wengine zilizokuwa zikifanywa na helikopta za utawala huo.
Ripoti za awali zinaonyesha kwamba askari wa miguu wa utawala wa Kizayuni wameshambuliwa na wapiganaji wa Hizbullah na kwamba helikopta za jeshi la Israel zilikuwa zikifanya shughuli za uokoaji katika maeneo ya mapigano ili kusafirisha maiti na wanajeshi waliojeruhiwa.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba walowezi milioni moja wamelazimika kukimbilia makazi yao kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora ya Hizbullah kwenye Bandari ya Haifa na eneo la Galilaya, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa.
Radio ya Israel imetangaza kwamba Ghuba ya Haifa, Galilaya Magharibi, na Galilaya ya Juu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) zimelengwa kwa mawimbi matatu ya mashambulizi ya makombora ya Hizbullah.
Manispaa ya Nahariya pia imewaomba walowezi wa Israel kuwa macho na kukaa karibu na maficho ya chini ya ardhi kutokana na uwezekano wa kuendelea mashambulizi ya makombora ya Hizbullah.
Wapiganaji wa Hizbullah wamekuwa wakijibu mashambulizi ya kikatili ya Israel ambayo imekiuka makubaliano ya kusitisha vita kwa kuendeleza mauaji ya raia wasio na hatia hasa kusini mwa Lebanon.