TAARIFA zilizoshtua ni zile za kuibuka kwa uvumi kwamba Simba ina mpango wa kutoendelea na aliyekuwa kipa wake namba moja kuanzia msimu uliopita na mwanzoni mwa msimu huu, Moussa Camara.
Camara yupo nje ya mfumo wa usajili wa Simba kuanzia Januari msimu huu, baada ya kuumia goti na kufanyiwa upasuaji. Simba ililazimika kumtoa nje ya mfumo wa usajili baada ya kutakiwa kupata muda wa kutosha kupona vyema jeraha, na hapo ndipo ilipomsajili Djibrilla Kasali, Januari kuziba nafasi pengo lake kwa muda.
Taarifa zinadai Kasali alipewa mkataba mfupi wa miezi sita ili kuona kama Camara ataweza kupona na kurudi kazini msimu ujao, ikizingatiwa kwamba tayari alishaanza mazoezi mepesi. Hata hivyo, siku za karibuni zimeibuka taarifa kwamba uwezekano wa Simba kumrudisha Camara ni mdogo na kwamba inatafuta kipa mwingine kwa msimu ujao, ikiwa na maana pia kwamba hata Kasali hayupo salama kwenye hesabu hizo.
AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI SHIRIKISHO CAF
Itakumbukwa mwanzoni mwa msimu uliopita, Simba ilimshusha Camara kuchukua nafasi ya Aishi Manula, na haraka alionyesha kiwango bora akiwavusha Wekundu wa Msimbazi kwenda hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ilitangulia kupoteza kwa mbaaoa 2-0 ugenini Aprili 2, 2025 dhidi ya Al Masry ya Misri, na mchezo wa marudiano Wekundu wakarudisha mabao hayo, Camara akiwavusha kwa kucheza penalti mbili kishujaa.
KINARA CLEEN SHEET
Msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwa Camara licha ya Simba kumaliza ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiukosa ubingwa kwenye mechi za mwisho, alifanikiwa kujibeba akimaliza kinara wa cleen sheet 19 kwenye michezo 30.
Namba hizo zilimfanya kuwa na ushawishi mkubwa wa kubeba tuzo ya kipa bora ambapo kama sherehe za ugawaji wa tuzo zingefanyika, alikuwa anabeba heshima hiyo akimbwaga Djigui Diarra wa Yanga, lakini pia akimzidi aliyekuwa anaishikilia Ley Matampi ambaye msimu mmoja uliopita alimaliza kinara na cleen sheet 15. Kwenye Shirikisho, Camara hakuruhusu mabao katika mechi nne kati ya 14 ya Simba, akiruhusu mabao tisa wakati Simba ikiishia fainali – ubingwa uliochukuliwa na RS Berkane ya Morocco.
YANGA YAMTIBULIA
Msimu uliopita, Simba ilipoteza mechi mbili nyumbani na ugenini kwenye ligi dhidi ya Yanga, na mchezo wa kwanza baina ya timu hizo Camara aliingia kwenye utata baada ya bao ambalo timu yake iliruhusu, akionekana kama alifanya kosa kwa kuurudisha mpira ndani ya uwanja wakati ulikuwa ukitoka nje.
Baada ya bao hilo, mmoja wa viongozi wa Simba, Crescentius Magori ambaye wakati huo alikuwa mshauri wa mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji alionyesha hadharani kutokubaliana na kiwango cha kipa huyo kwenye mchezo huo. Hata hivyo, Camara baadaye alirudi na kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo iliyofuata ikiwemo dhidi ya Al Masry ambayo aliitumia kuibeba Simba na kuipeleka nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya Camara kuonyesha kiwango bora, lakini alijikuta njiapanda kupewa mkataba mpya ambapo uliibuka mjadala wa utata kama ataongezewa muda wa kuendelea kulinda lango la Wekundu wa Msimbazi. Hata hivyo, aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids, alimaliza utata huo akiwataka mabosi kuendelea na kipa huyo, kisha akapewa mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika mwisho wa msimu huu.
Ubora zaidi wa Camara ni kwamba akiwa Simba aliendelea kulinda nafasi yake akiwa pia kipa chaguo la kwanza kwa taifa lake la Guinea.
KIVULI CHA DIARRA, MANULA
Kwa ujumla kwa hesabu za namba na takwimu za kipa huyo, viwango vya makipa waliopo Simba kwa sasa hakuna ambaye anaweza kumzidi, lakini kama akilinganishwa na makipa wa nje na klabu hiyo pengine inaweza kuwa shida. Simba wakati inatafuta utulivu wa eneo la makipa inatakiwa kuhakikisha hairudii makosa ambayo iliyafanya kwa Aishi Manula, ambaye licha ya kurudishwa chini na kuinuliwa kwa Camara wakati wawili hao wakiwa wote Simba, lakini aligoma kupotea.
Manula amerudi kwenye ubora wake akiwa imara langoni, lakini bahati ni kwamba kiwango hicho sasa anakionyesha akiwa na timu yake ya zamani, Azam FC, huku akiiumiza Simba ambayo imeyumba kwa ubora wa makipa waliosalia.
Endapo Simba ingekuwa na utulivu wa uamuzi, wakati huu inapata shida na suala la jeraha la Camara, basi Manula angeendelea kuonyesha ubora wake wa sasa akiwa na Wekundu wa Msimbazi.