
Hivi karibuni nilimsikia jamaa mmoja kwenye moja ya vikao vya wanaume akisema:“Hakuna mtoto anaweza kulelewa vizuri akawa binadamu bila baba. Twende mbele turudi nyuma, malezi hayakamiliki bila baba.”
Ingawa alishangiliwa sana na hadhira yake kwa kuonekana kuulinda uanaume kwa nguvu zote, maneno hayo yalinitafakarisha sana hasa alipoongeza kusema:
“Wanawake wenyewe ndio hawa wanataka kutupandia vichwani? Unazaa naye anataka tena kukutawala unamwachia mtoto ili ajifunze kwa machozi kuwa bila baba hata huyo mtoto anayeringa naye hawezi kuwa mtu.”
Kauli kama hizi zinaweza kuwa maarufu kwenye vikao vya wanaume, lakini ukweli zina uwezo wa kutengeneza tatizo kubwa huko tuendako.
Mama ndiye msingi mkuu wa malezi tangu mwanzo. Tangu mtoto akiwa tumboni hadi miaka mitatu ya mwanzo, mama kupitia uhusiano wake na mtoto, ndiye anayeamua mtoto anajionaje, anawaonaje watu na anayachukuliaje maisha.
Wanasaikolojia, John Bowlby na Mary Ainsworth waligundua kuwa mtoto anapokuwa na uhusiano unaomhakikishia usalama katika umri mdogo, safari ya maisha yake inakuwa yenye afya na amani.
Mtoto huyu anapokutana na changamoto zozote za maisha, akili yake hurejea kumbukumbu yake ya usalama aliyowahi kujisikia akiwa na mama yake. Mtoto wa namna hii, hata pale anapohisi hatari, bado hujenga hali ya kujiamini na ustahimilivu wa kihisia.
Kisayansi mama ndiye anayekuwa egemeo kuu la malezi hata kwenye familia zenye baba. Kinachoamua namna mtoto atakavyokabiliana na changamoto za maisha, ikiwemo ombwe la kumkosa baba, ni aina ya uhusiano aliokuwa nao na mama yake.
Nafasi ya baba
Baba ana nafasi muhimu katika malezi. Kisayansi, tunaambiwa, anayemsaidia mtoto kujifunza namna ya kudhibiti hisia kali, kujenga nidhamu ya mtoto na wakati mwingine kujifunza namna jinsi mbili zinavyohusiana ni baba.
Utafiti mwingi unaonesha kuwa kukosekana kwa baba, kunaweza kuathiri hali ya mtoto kujiamini, uhusiano wake wa baadaye, na hata uwezo wake wa kurekebisha hisia.
Kadhalika, katika mazingira haya, mtoto anaweza kuwa na ombwe la kukosa mwanaume wa kujifunza kwake, ombwe ambalo linaweza kumfanya akose utulivu kwenye uhusiano.
Hata hivyo, hiyo haimaanishi kuwa mama akiwa pekee hawezi kumlea mtoto wake vizuri. Namna gani mama anasimama kwenye nafasi yake, anashirikiana na familia pana na kupata usaidizi wa jamii, ndivyo hasa vinavyoamua uwezo wa mtoto kukabiliana na pengo hilo la kumkosa baba.
Ingawa baba ana umuhimu wake katika malezi, yapo mazingira huwa juu ya uwezo wa mama yanayomfanya asiwe na uchaguzi mwingine zaidi ya kuwa mlezi wa pekee yake.
Kumgeuza mwanamke kuwa ndiye chanzo cha matatizo uhusiano ‘unapoparaganyika’ ni kukosa uelewa mpana wa uhusiano. Vipi kuhusu wanaume wanaokimbia ujauzito na kuwalazimisha wanawake kutoa mimba?
Utasema ni kiburi cha mwanamke? Vipi wanaume wanaowakataa watoto ili kulinda ‘heshima’ zao katika jamii? Utasema ni kiburi? Tukubaliane kuwa wanawake hukutana na wanaume wengi wasiojitambua ambao, badala ya kuwa nguzo, hugeuka kuwa chanzo cha maumivu ya kiuchumi, kihisia, kijamii na hata kiroho kwa wanawake. Uanaume haulindwi kwa kuwasitiri wanaume hawa wanaowafanya wanawake wapambane na unyanyapaa wa jamii unaombebesha mwanamke lawama.
Mwanamke ufanye nini?
Mwanamke anaweza kufanya nini katika mazingira haya ya ombwe la ubaba? Kuna wanaofikiri labda mama awe na ratiba nzuri zaidi inayomuweka karibu na mwanawe kumpa utulivu unaomfanya ajisikie salama.
Wengine wanafikiri mama apambane kujitunza na kuzungumza na wengine, kama namna ya kumpa nguvu zaidi ya kutoa malezi yenye ubora.
Kadhalika, mama afanye mazungumzo ya wazi na mtoto kumsaidia kuelewa na kukubali hali ya kumkosa baba bila kujenga uhasama na baba yao.
Inawezekana pia “kijiji” kinachotajwa katika methali zetu kinaweza kutusaidia. Tunao wanaume kama baba mkubwa, mjomba, binamu na wengine wanaoweza kuwa mifano bora kwa mtoto na kujaza ombwe la baba.
Jingine ni uhuru wa mmwanamke kiuchumi. Umasikini unaweza kuwa sawa na chumvi kwenye kidonda. Mwanamke anapojitegemea kiuchumi akawa na kipato cha uhakika, inasaidia kumpa nguvu zaidi ya kubeba majukumu ya malezi bila kutegemea watu ambao wakati mwingine hawako tayari kuona akijitegemea.
Inawezekana mama kumlea mtoto bila msaada wa karibu wa mwanaume. Ingawa tungetamani mtoto alelewe na wazazi wote wawili, inapotokea mama analazimika kuwa mzazi pekee, bado sayansi inaonesha kuwa analo tumaini.
Mama anapojijenga kihisia, akakubali hali yake, akaufaa ujasiri wa kuyakabili maisha bila kutegemea huruma ya watu ambao wakati mwingine wanatumia hali yake kumnyanyapaa, anaweza kabisa kumlea mtoto vizuri na akawa binadamu mwema bila kuwa na baba.