BEKI wa Kitanzania, Abdulmalik Kajuna anayekipiga  Psalms 105 FC inayoshiriki Ligi Daraja la pili Kenya amesema tofauti kubwa kati ya ligi ya huko na Tanzania ni fedha.

Kajuna amesema Kenya vipaji vinapewa sana nafasi lakini pesa ndo tatizo tofauti na Tanzania na Ligi Kuu Bara imekuwa na uwekezaji mkubwa zaidi ya Kenya.

“Huku Kenya wanathamini vipaji, hawatangulizi pesa mbele. Kuna muda hali inakuwa ngumu lakini tunavumilia. Tanzania mara nyingi wanaangalia pesa kwanza kuliko vipaji,” amesema.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 19, anaamini kucheza katika mazingira tofauti Kenya kumemjenga kiushindani na kumpa uzoefu mkubwa  anaoamini utamfungulia milango ya kucheza soka la kiwango cha juu zaidi.

Kwa sasa timu hiyo iko kwenye nafasi nzuri  ya kuwania mbio za kupanda daraja kutokana na mwenendo mzuri msimu huu.

“Nimecheza mechi 16, nne sijacheza. Tumepoteza mchezo mmoja tu na tunaongoza ligi. Mungu akijalia tumebakiza mechi moja tupande daraja,” amesema.

Kajuna ambaye ana uwezo wa kucheza beki wa kati na beki wa kulia, amesema safari yake imekuwa na changamoto nyingi lakini bado anaamini atafikia mafanikio makubwa kutokana na kipaji chake.

Nyota huyo aliyezaliwa Kahama, mkoani Shinyanga amesema alianza kucheza soka kwenye ligi za chini, kabla ya kupata nafasi ya kwenda Kenya. Awali aliichezea Azania FC katika ligi ya wilaya kabla ya kujiunga na Ambassador FC kwenye ligi ya mkoa.

“Kahama ligi ya wilaya nilicheza mechi zote hadi tukawa washindi wa pili nikiwa Azania FC.

“Pia nikacheza ligi ya mkoa mechi tano nikiwa Ambassador FC kabla sijapata nafasi ya kuja Kenya,” amesema Kajuna.

Mwaka 2021 alipata nafasi ya kujiunga na Muhoroni Youth FC na alianza kucheza soka la ushindani zaidi Kenya na akiwa huko alipata nafasi ya kucheza timu zote mbili za klabu hiyo zilizokuwa zikishiriki Ligi Kuu na Ligi Daraja la Pili.

“Nilicheza misimu miwili Muhoroni Youth. Timu ilikuwa na kikosi cha Ligi Kuu na Daraja la Pili, hivyo nilipata nafasi ya kucheza kote,” amesema.

Baada ya hapo alihamia Home Stars FC msimu wa 2023/24 na alicheza mechi zote na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu kwenye ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *