Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, amesema maridhiano ni msingi muhimu wa kujenga jamii salama, yenye ustaarabu na inayothamini maisha ya binadamu.
Amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika Kongamano la 31 la Kimataifa la Qur’an na Hadithi la Al-Mustafa, lililofanyika Kigamboni,Leo Mei 10, 2026 Kigamboni Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini.
Sheikh Salum alirejea matokeo ya ripoti ya Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande, iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026, kuhusu vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya Oktoba 29, 2025.
Amesema hata mataifa makubwa duniani hutumia mazungumzo na maridhiano kama njia ya kuzuia migogoro na kulinda maisha ya watu.
Baadhi ya waumini waliojitokeza kwenye Kongamano la 31 la Kimataifa la Qur’an na Hadithi la Al-Mustafa, lililofanyika Kigamboni,Leo Mei 10, 2026 na kuhudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini.
“Maridhiano ni jambo jema kwa jamii iliyostaarabika. Watanzania wanahitaji maridhiano kutokana na mpasuko uliojitokeza ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi,” amesema Sheikh Salum.
Amesema mafundisho ya Qur’an yana mchango mkubwa katika kujenga maadili kwa vijana na kuimarisha uzalendo, akisisitiza kuwa mtu anayezingatia maadili ya Qur’an hawezi kuwa chanzo cha vurugu au uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Al-Mustafa International Foundation Dar es Salaam, Dk Ali Tagavi, alisema mashindano hayo ya Qur’an yalianza miezi mitatu iliyopita na kufikia kilele chake kwa washindi kutunukiwa tiketi za kwenda Hijja.
Baadhi ya waumini waliojitokeza kwenye Kongamano la 31 la Kimataifa la Qur’an na Hadithi la Al-Mustafa, lililofanyika Kigamboni,Leo Mei 10, 2026 na kuhudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini.
“Tunawashukuru washiriki wote pamoja na wageni mbalimbali waliofanikisha kongamano hili ambalo limekuwa kilele cha mashindano hayo,” amesema Dk Tagavi.
Naye Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC), Hemed Jalala, amesema kongamano hilo limewakutanisha Watanzania wa imani tofauti kwa lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na uvumilivu katika jamii.
Amesema mafundisho ya Qur’an yanasisitiza watu kuvumiliana, kusameheana na kutatua changamoto kwa mazungumzo na mshikamano.
Miongoni mwa waliohudhuria kongamano hilo alikuwa mfanyabiashara Azim Dewji, ambaye amesema mafundisho ya dini yana mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili na amani.
“Watoto wanaojifunza Qur’an hujengwa katika misingi ya wema na nidhamu. Jamii ikithamini dini na maadili, kutakuwa na amani na kuepukwa kwa migogoro,” amesema Azim Dewji.