Dar es Salaam. Dhamira ya Tanzania ya kuongeza idadi ya kaya zinazotumia nishati safi ya kupikia inategemea kwa kiasi kikubwa uwekezaji wenye tija na unaojibu mahitaji halisi katika sekta ya nishati, wabunge wamesema.

Serikali ilipitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (NSCCE 2024–2034) mwaka 2024, ukiwa na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia sita wakati huo hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Kiwango hicho kimeongezeka hadi kufikia takribani asilimia 24, lakini wabunge wanasema bado juhudi kubwa zinahitajika ili kufikia lengo hilo, ikiwamo kuhakikisha uwekezaji unaolenga moja kwa moja kutatua changamoto za nishati na mazingira.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati, matumizi ya mkaa, kuni na mabaki ya mazao yanaendelea kusababisha madhara makubwa kiafya, yakichangia vifo vya watu hadi 33,000 kila mwaka.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited, jijini Dar es Salaam  Mei 10, 2026 kwa lengo la kujionea uwekezaji unaofanywa na kampuni iyo nchini.

Takwimu za wizara za mwaka 2022, zinaonyesha mtu anayevuta moshi wa kuni kwa saa moja huwa katika hatari sawa kiafya na mtu anayevuta sigara kati ya 200 hadi 300.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema wawekezaji katika sekta hiyo wanapaswa kuhakikisha uwekezaji wao unanufaisha Taifa, unazingatia sheria za nchi na kuweka mbele masilahi ya wananchi.

Kamati hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Subira Mgalu walipotembelea mitambo ya vilainishi na gesi ya LPG inayomilikiwa na Oryx Energies Tanzania jijini Dar es Salaam jana Jumamosi.

Mgalu amesema kamati inatambua mchango mkubwa wa Oryx Energies, katika kipindi cha miaka minne kampuni hiyo imechangia pato la Taifa la Sh1.2 trilioni huku ikitoa ajira za moja kwa moja 1,000, wengi wao wakiwa vijana wa Kitanzania.

“Kwa uwepo wake wa miaka 25 nchini, Oryx Energies imekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha Watanzania kupata ajira, pia imechangia maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Taifa,” amesema Mgalu.

Amesema wabunge wameona baadhi ya mafanikio ya kampuni, ikiwamo maabara za kisasa kwa ajili ya kupima ubora wa vilainishi. Vilevile, matumizi ya nishati safi ya kupikia nyumbani yameongezeka kutoka asilimia 6 awali hadi kufikia asilimia 26, na ongezeko hili lina mchango mkubwa kutoka Oryx na wadau wengine.

Mgalu pia amemsifu Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hatua inayotambulika kimataifa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited, jijini Dar es Salaam  Mei 10, 2026 kwa lengo la kujionea uwekezaji unaofanywa na kampuni iyo nchini.

“Kamati hii inaendelea kusisitiza uwekezaji unaotoa tija na matokeo chanya kwa Taifa letu, hasa katika kuinua uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Limited, Imani Mtafya amesema uwepo wa kampuni kwa miaka 25 umesaidia Watanzania kuhakikisha wanapata bidhaa bora, hususan vilainishi.

Aidha, kampuni inachangia Sh300 bilioni kila mwaka sawa na asilimia 0.1 ya pato la taifa, huku asilimia 99 ya wafanyakazi wake wakitoka nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania, Benoite Araman ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kampuni kuunga mkono sera za Serikali zinazolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *